Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) imesema waathirika wote wa ajali iliyotokea mkoani Morogoro hivi karibuni na kusababisha vifo vya watu 23 watalipwa fidia stahiki kwa mujibu wa sheria mara baada ya taratibu za kipolisi na kibima kukamilika.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano cha Tira, imemnukuu Kamishna wa Bima Tanzania, Dk Baghayo Saqware ikieleza kuwa, mamlaka hiyo inatambua kuwa basi lenye namba za usajili T 732 ATH lilikuwa lina bima hai na halali.
“Ni ajali mbaya na Tira itahakikisha haki inapatikana kwa kila aliye athirika na ajali hii kwa kuwa basi lilikuwa na bima halali na hivyo ni haki yao wote waliohusika kwenye ajali kupatiwa stahiki zao, hivyo taratibu za kibima, kipolisi zikikamilika, Tira itahakikisha wote wanalipwa,” alisema Saqware.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu, ajali hiyo ilitokea saa 10:30 jioni baada ya basi hilo linalomilikiwa na kampuni ya Ahmeed Coach kugongana uso kwa uso na lori katika eneo la Melela Kibaoni, Wilaya ya Mvomero, barabara kuu ya Iringa-Morogoro.