Serikali imesema itaanza kuwafikia vijana ambao hawakuwa wamefikisha umri wa kupata chanjo ya Uviko-19 tangu zoezi hilo lianze miaka mitatu iliyopita ambao kwa sasa watakuwa wametimiza miaka 18.
Pia iko mbioni kuanza kutoa chanjo za kusisimua (booster) za Uviko-19 kwa watu wote waliochanja chanjo za kukabiliana na ugonjwa huo.
Mratibu wa chanjo Mkoa wa Mwanza, Amos Kitereja akizungumza na waandishi wa habari Januari 13 jijini Mwanza amesema lengo ni kuhakikisha wote waliopata chanjo mbalimbali na ambao hawakupata wanapatiwa kwa pamoja.
Kitereja pia amesema katika mpango huo wataweka msisitizo kwa wilaya ambazo zipo chini kwenye suala la uchanjaji ili ziweze kufikia lengo la kuchanja.
“Lengo tunatamani kuwapatia chanjo wote ambao hawajapatiwa chanjo na hasa wale ambao walikuwa chini ya miaka 18 wakati zoezi linaanza ambapo kwa sasa watakuwa wamefikisha umri wa kuchanja,” amesema Kitereja.
Kwa mujibu wa Kitereja amesema Mkoa wa Mwanza unakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni 4 na kati ya hao watu milioni 1.8 ni vijana wenye umri wa miaka 18.
“Tunataka sasa kuwahamasisha hao vijana nao waweze kupatiwa chanjo ya Uviko-19 hivyo ni jukumu la kila mmoja vikiwemo vyombo vya habari kuhakikisha vinatoa elimu ya kuhamasisha watu kwenda kuchanja,” amesema Kitereja.
Amesema mpaka sasa mkoa umefanikiwa kuchanja kwa asilimia 100 ambapo waliochanja chanjo zaidi ya moja ni asilimia 102 huku waliochanja chanjo moja wakiwa ni asilimia 125.
Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Dk Silas Wambura amesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba mwaka huu, mkoa huo ulikusudia kuchanja watu watu 1.2 milioni.
Amesema hadi zoezi linakamilika walikuwa wamefanikiwa kuchanja kwa asilimia 100.