Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imependekeza kwamba magari yatakayopita kwenye daraja la Tanzanite (Daraja jipya la Salenda) jiji Dar es Salaam yatozwe ushuru.
Kamati hiyo imesema ushuru uwepo katika daraja hilo kama ilivyo kwa daraja la Nyerere (Kigamboni) kwani daraja la Tanzanite nalo limejengwa kwa fedha za mkopo.
“Kamati inaitaka Serikali pindi daraja hili litakapokamilika, kwa sababu limejengwa kwa mkopo kama lilivyo Daraja la Kigamboni, liwe ni daraja la kulipia yaani” amesema Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Sillo Baran.
Ujenzi wa daraja hilo ulizinduliwa Julai 23, 2018 na aliyekuwa Rais wakati huo, Hayati John Pombe Magufuli ikiwa ni mpango wa kupunguza msongamano wa magari katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Barabara ya Barack Obama.
Jana Rais Samia Suluhu alisema daraja hilo lenye urefu wa kilomita 1.03 na upata wa mita 20.5 linatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2021 na kuzinduliwa katika sherehe za miaka 60 ya Uhuru.