Miaka miwili baada ya watalii kutoka nchini Italia kusitisha safari zao kwenda Zanzibar kutokana na janga la Uviko-19, safari hizo zimerejea baada ya shirika la ndege la Neoes nchini humo kuwasili na watalii 320 kisiwani humo.
Safari za moja kwa moja kutoka Italia kwenda Zanzibar zilisitishwa tangu Machi, mwaka 2020 kutokana na janga hilo.
Watalii hao waliambata na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mahmod Thabit Komdo walifika juzi na kupokelewa na viongozi mbalimbali katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohamed Said alisema Zanzibar inaunga mkono jitihada za mataifa kuhusu hatua hiyo ya kurejesha watalii nchini.
Naye Balozi Kombo alisema wanategemea ndege zaidi za kitalii kutua Zanzibar, ikiwemo Serbia na Crotia, huku akiwataka wahusika kuharakisha vibali vya kuingia nchini kwa mashirika ya ndege.