Waziri Mkuu asimamisha kazi watumishi 9

HomeKitaifa

Waziri Mkuu asimamisha kazi watumishi 9

Waziri Mkuu wa, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri na watumishi wengine tisa wa jiji hilo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa Sh10 bilioni za Serikali ambazo zilikusanywa na hazikuwasilishwa benki kama sheria inavyoelekeza.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Julai 11, 2022 imesema agizo hilo linatokana na matokeo ya ukaguzi maalumu kuhusu Mapato ya Ndani katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2020/2021 uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Majaliwa ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na  viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, wabunge, madiwani pamoja na watumishi wa wilaya ya Ilala katika ukumbi wa Karimjee akiwa katika ziara yake ya kikazi Dar es Salaam.

Watumishi hao pia wamekabidhiwa kwa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dar Es Salaam kwa mahojiano juu ya tuhuma zinazowakabili.

Majaliwa amesema mbali na Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam, watumishi wengine ni pamoja na Tulusubya Kamalamo (Mweka Hazina), James Bangu (Mhasibu Mapato), Abdallah Mlwale (Mtunza Fedha Mkuu) na Mohammed Khais (Mhasibu wa Masoko).

Majaliwa ametaja watumishi wengine wanaopaswa kuchukuliwa hatua kuwa ni Jesca Lugonzigwa (Afisa Hesabu), Josephine Sandewa (Afisa Hesabu), Tatu Mkangwa (Kibarua) na Felician Maro (Mhasibu Msaidizi) ambao wameisababishia halmashauri hasara ya shilingi 1,214,907,637.

“Watumishi hao wanatuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na hivyo kuisababishia halmashauri hasara ya jumla ya kiasi cha shilingi 10,137,577,401 zilizokusanywa na mawakala na watumishi wa Halmashauri hiyo lakini hazikuingizwa benki”.

Waziri Mkuu amesema Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwepo kwa umakini kwenye ukusanyaji na matumizi ya mapato ili kuiwezesha Serikali kuendelea kujenga miradi mingi zaidi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. “Ilala pamoja na kupata hati safi lakini ndani yake kuna mambo ambayo hayana tija.”

Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ufuatilie vyanzo vyote vya mapato vya halmashauri hiyo na pia waweke makadirio ambayo yatawawezesha kukusanya zaidi. Pia amewasisitiza waweke makadirio yatakayowawezesha kufanya kazi zaidi na kila muhusika ahakikishe anatekeleza majukumu yake ipasavyo.

error: Content is protected !!