Waziri wa Fedha akaangwa na wafanyabiashara Kariakoo

HomeKitaifa

Waziri wa Fedha akaangwa na wafanyabiashara Kariakoo

Baadhi ya wafanyabiashara nchini Tanzania wamesema hawaridhiishwi na namna Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba anavyoshughulikia changamoto zinazowakabili ikiwemo uanzishwaji wa sheria zinazowaumiza bila kufungua milango ya majadiliano.

Mwenyekiti wa Wamiliki wa Malori Madogo na ya Kati Tanzania, Chuki Shabani ambaye aliyekuwa akizungumza kwenye mkutano kati ya Wafanyabiashara na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana Mei 17 amesema kuwa hawafurahishwi na utaratibu wa kutunga sheria za kodi bila wao kutoa maoni.

“Wanatuita kwenye vikao vya kamati, wakati sisi tunatoa maoni wao wanapitisha sheria, unapitishaje sheria jambo ambalo bado watu hawajalitolea maoni.. Hiki kiburi cha Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) kinatokana na bosi wao,” amesema Shabani.

Shabani amedai kuwa waziri huyo hawezi kupokea maoni ya wananchi wa kawaida kwani ameshaonesha kuwadharau wabunge wenzake ndani ya Bunge la Tanzania kwa kutoa kauli zisizo za kiungwana pale alipopewa maoni kwa ‘kuwaita waganga wa kienyeji.’

Itakumbukwa Februari Mosi 2023, Waziri Mwigulu alipokuwa akichangia katika taarifa ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira aliwataka Wabunge kujadili mambo mengine yanayohusu uganga wa kienyeji na mambo mengine na kueleza kuwa kwenye uchumi ni umahiri wake.

“Hebu tujadilini mambo mengine mengine huko yanayohusu uganga wa kienyeji kwenye uchumi hii ni taaluma yangu,” alisema Nchemba

Hata hivyo kauli hiyo ilifutwa kwenye kumbukumbu za Bunge baada ya Wabunge kulalamikia kauli hiyo.

Baadhi ya wafanyabiashara katika mkutano wamesema hawaamini kama maoni waliyotoa kuhusu kodi yatafanyiwa kazi na Waziri Nchemba wakidai hawana imani naye huku wakitaka ajitafakari kama anastahili kuendelea kuwepo katika nafasi yake.

Usimamizi mbaya wa Fedha

Wafanyabiashara wamebainisha kuwa wanasikitishwa na vitendo vya ubadhirifu na upotevu wa fedha unaotokea serikalini ambapo kwa kiasi kikubwa zinatokana na kodi ambazo wao wanazitoa na kumtaka awadhibiti wanaosababisha upotevu huo.

“Utaendelea kutuumiza sisi, tutaumia na tunaumia chonde chonde (Waziri Mwigulu) elekeza udhibiti wako kwa hao wanaosababisha ubadhirifu, tutapata wapi moyo sisi wafanyabiashara kulipa kodi huku tunasikia Sh2 trilioni zimepigwa,” amesikika mfanyabiashara mmoja.

Baadhi wapongeza

Wakati wengine wakionesha kutokuridhishwa na utendaji wa Waziri Mwigulu baadhi wameonekana kuridhishwa akiwemo Yusuph Oyenga kutoka Dar es Salaam ambaye amesema anatambua utendaji wa kazi wa Mwigulu ila kilichotokea ni ajali kazini ingawa wafanyabiashara walio wengi hawakukubaliana na kauli hiyo.

“Tunamshukuru mheshimiwa Rais kurusu hali hii na kukuruhusu wewe waziri wake mkuu , na mawaziri wanne waandamizi kuwepo hapa, kaka yangu Mwigulu Waziri wangu wa fedha hizi ni changamoto za kazi najua uwezo wako wa kazi,” amesema Oyenga.

Waziri wa Viwanda naye aguswa

Pamoja na kutofurahishwa na matendo ya Mwigulu, Shaban alitema nyongo kwa kuelezea kutopendezwa kwa kitendo cha Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk Ashatu Kijaji ambaye aliwaambia Wabunge baadhi ya wafanyabishara wamefungua maduka yao na waliogoma wamefanya hivyo kwa hiyari.

“Kwa kweli tumesikitika sana baada ya kuona Waziri wa Viwanda na Biashara hatilii maanani kile kinachoendelea Kariakoo, bila kujali kwamba watu wanaumia, kodi zinaumiza,” amesema mfanyabiashara huyo huku akipigiwa makofi

Wafanyabiashara wa soko la Kariakoo wamekutana na Waziri Mkuu wa Tanzania kujadili changamoto zinazowakabili kufuatia mgomo wa siku mbili, ambapo wamealikwa wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali kuelezea changamoto za kikodi zinazowakabili.

Waziri Mkuu ameambatana na mawaziri wa kisekta akiwemo Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Biashara Ashatu Kijaji, pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni ambao wanasikiliza changamoto zinazotajwa na wafanyabiashara hao ili kuzifanyia kazi.

Mazungumzo haya yanakuja baada ya wafanyabiashara wa soko la Kariakoo kugoma kufungua maduka yao kwa siku tatu mfululizo wakigomea utekelezaji wa kodi ya ghala, kamata kamata ya wafanyabiashara pamoja na ushuru wa forodha.

error: Content is protected !!