Yohane Lauwo: ‘Guide’ wa kwanza kumpandisha mzungu mlima Kilimanjaro

HomeUncategorized

Yohane Lauwo: ‘Guide’ wa kwanza kumpandisha mzungu mlima Kilimanjaro

Tumefundishwa shuleni kuhusu Hans Meyer kuwa mzungu wa kwanza kupanda Mlima Kilimanjaro 1889, lakini hatujui kwanini Yohani Lauwo amesahaulika, hatujajua bado kwanini mtu huyu ni mgeni sana masikioni mwa walio wengi.

Kwa wakati huo Hans Meyer alipofika Kilimanjaro, ingalikuwa ngumu sana kwake kujua njia za mlimani, hekaheka zake na kila kitu kuhusu mlima kama asingelipewa msaada. Lakini historia kubwa inamhadithia Hans.

Yohane Kinyala Lauwo, alikuwa na umri wa miaka 19 tu wakati Hans Meyer na mwenzake Ludwing Purtscheller walipofika kupanda hadi kileleni mwa Mlima Kilimanjaro October 15 1889. Yohane inasemekana aliteuliwa tu bila kukusudiwa kumuongoza Hans mlimani na Rais wa Wa Chagga (Mangi). Yohane yeye na familia yake waliishi Marangu kandokando ya mlima, na shughuli yao kubwa ilikuwa ni kuwinda tendo ili kujipatia pembe na kuwauzia waswahili kutoka Pwani.

Yohane aliujua vyema msitu na mazingira yake, alitambua dawa za asili na humo akapata chakula kama asali na rasilimali kama mbao. Ukoloni ulishaanza kushamiri kwa kasi Kilimanjaro wakati huo, hivyo vijana wengi wa marika ya Yohane walikuwa wanakamatwa na kulazimishwa kufanya kazi kama za kuchonga barabara na nyinginezo.

Yohane hakuwa tayari hivyo akawa mtoro na mkwepaji, bahati mbaya alikamatwa na kufikishwa mbele ya Mangi Marealli. Muda huohuo Hans Meyer akafika kwa Mangi kutaka kibali cha kupanda mlima. Moja ya washauri wa karibu wa Mangi alikuwepo, akamtazama Yohane akashauri kijana ampeleke Hans mlimani.

Safari yake ya kwanza kama ‘guide’ mlimani, ilimfanya kuwa guide kwa miaka 70. Siku ya kwanza alipanda akiwa amejifunika blanketi tu, siku za mbele akiwa mpanda mlima rasmi akapata mavazi mazuri ya kumlinda na baridi ya mlimani.

Alipohitimu miaka 100, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania ikampatia nyumba nzuri ya kisasa ambayo aliishi na wakeze wawili, aliishi hapo hadi alipofariki tarehe 10 Mei 1996 akiwa na umri wa miaka 120.

error: Content is protected !!