Zaidi ya shule 20,000 za msingi na 5,000 za sekondari zina vyanzo vya maji vya uhakika

HomeElimu

Zaidi ya shule 20,000 za msingi na 5,000 za sekondari zina vyanzo vya maji vya uhakika

Serikali imesema kuwa shule 5,311 za Sekondari zina vyanzo vya maji vya uhakika, huku pia shule 20,509 za msingi zina vyanzo vya maji ya uhakika.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), Festo Dugange alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Fiyao aliyehoji lini serikali itaanza kujenga mifumo ya uvunaji wa maji ya mvua katika shule zote nchini.

“Sensa ya ElimuMsingi Mwaka 2024 inaonesha kuwa shule 5,311 za Sekondari zina vyanzo vya maji vya uhakika ambapo shule zenye maji ya bomba ni 2,960, visima shule 1,217 na wanaovuna maji ya mvua ni shule 1,134.

“Aidha, shule 20,509 za msingi zina vyanzo vya maji ya uhakika ambapo shule zenye maji ya bomba ni 10,965, visima shule 4,966 na shule zinazovuna maji ya mvua ni 4,578,” amesema.

Amesema mikakati ya Serikali ya kufikisha huduma za maji safi na salama katika shule za msingi na sekondari nchini ni pamoja na ujenzi wa shule mpya au miundombinu ya vyoo kujumuisha fedha za ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua.

“Serikali kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa itaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha shule zinakuwa na huduma ya maji safi na salama kwa kuzingatia vyanzo vya maji vya eneo husika,” amesema Naibu Waziri.

error: Content is protected !!