Zaidi ya watainiwa 270 wafutiwa matokeo darasa la nne, kidato cha pili

HomeKitaifa

Zaidi ya watainiwa 270 wafutiwa matokeo darasa la nne, kidato cha pili

Udanganyifu katika vyumba vya mitihani umewaponza watahiniwa 279 wa kidato cha pili na darasa la nne mwaka jana kutokana na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kufuta matokeo yao baada kugundulika kufanya vitendo hivyo.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta Athumani Amasi aliyekuwa akisoma matokeo ya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne na kitato cha pili mwaka 2022  amewaambia wanahabari kuwa watahiniwa hao wamefutiwa matokeo kutokana na kubainika kufanya udanganyifu na kuandika matusi.

Kati yao waliofutiwa matokeo, 213 ni wa darasa la nne na 66 wa kidato cha pili jambo ambalo ni kinyume cha kanuni na sheria.

“Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 (2) (i) cha Sheria ya Necta sura ya 107 kikisomwa pamoja na kifungu ch 30(2) (b) cha Kanuni za Mitihani mwaka 2016,” amesema Amasi katika ofisi za Necta jijini Dar es Salaam.

Licha ya hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali bado vitendo vya udanganyifu wa mitihani vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara na kutia doa mchakato huo unaotumainiwa kupima uelewa wa wanafunzi.

Mapema Mwezi Disemba mwaka 2022, Necta ilifuta matokeo ya wanafunzi 2,194, sawa na asilimia 0.16 ya watahiniwa milioni 1.3, baada ya kubainika kufanya udanganyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2022.

Itakumbukwa Oktoba 25 mwaka 2022 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliagiza kufungwa kwa Shule ya Chalinze Modern Islamic Pre and Primary iliyoko mkoani Pwani kuwa kituo cha mtihani kwa muda usiojulikana baada ya kubainika kufanya ufanganyifu kwenye mtihani wa darasa la saba.

Matokeo yaliyozuiliwa

Pamoja na kufuta matokeo, Necta imezuia matokeo ya watahiniwa 442 katika mtihani wa darasa la nne na 258 wa kidato cha pili ambao walipata matatizo ya kiafya.

“Wanafunzi husika wamepewa fursa ya kufanya upimaji  kwa masomo ambayo hawakuyafanya kwa sababu ya ugonjwa mwaka 2023 kwa mujibu wa kifungu cha kanuni 32 (1) cha Kanuni za Mitihani,” amesema Amasi.

Aidha, Necta imefungia vituo viwili vya mitihani ambavyo ni Shule ya Msingi Busara na Mugabe zote za Mkoani Mwanza baada ya kuthibitika kufanya udanganyifu katika mtihani wa darasa la nne.

Hii si mara ya kwanza kwa Mkoa wa Mwanza kuwa na vituo ambavyo vimefungwa kutokana na udanganyifu. Katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana, Mkoa wa Mwanza ndiyo uliongoza kwa kuwa na vituo vingi vya mitihani vilivyofungiwa kwa kuwa na shule tisa kati ya 26.

error: Content is protected !!