Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kutumia teknolojia ya skana za EDE kupima Uviko-19 kwa wasafiri wanaowasili na kusafiri kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Skana za EDE hupima kwa kutumia simu ya mkononi na kifaa kingine maalumu ni maarufu katika mataifa ya falme za kiarabu na hutumia sekunde tatu tu kujua hali ya mtu na kumpatia majibu yake.
Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi alisema kwamba teknolojia hiyo imekuja sambamba na kurejea kwa ndege za mashirika yaliyopo falme za kiarabu ambayo miongoni mwa makubaliano ya kurejea ni kuwahakikisha kipimo hicho ambacho hakina usumbufu.
“Serikali haijalipia teknolojia hii lakini imekuja kutokana na uhusiano mzuri uliopo, ni imani kuwa ikionyesha matokeo chanya na mataifa mengine hususani ukanda wa Afrika Mashariki yatafuata hatua hiyo. Zanzibar inategemea utalii hivyo inafanya kila jitihada kuhakikisha shuguli hizo zinaendelea,” alisema Rais Mwinyi.
Zanzibar inakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kutumia teknolojia hiyo kutoka Abu Dhabi.