TMA yatangaza ujio wa mvua kubwa

HomeKitaifa

TMA yatangaza ujio wa mvua kubwa

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya ujio wa mvua kubwa za wastani mpaka juu ya wastani katika kipindi cha masika (Machi-Mei) kwa mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka.

Mkurugenzi wa TMA, Dk. Agnes Kijazi alisema mikoa yote inayopata mvua hizo inatarajiwa kuwa na mvua kubwa na hivyo kutoa tahadhari kwa sekta mbalimbali kuchukua hatua kukabiliana na athari zinazoweza kutokea kutokana na uwapo wa mvua hiyo.

“Mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwapo kwa mvua kubwa katika msimu huu wa masika na zitaanza kunyesha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Februari na kumalizika mwezi Mei,” alisema Dk. Kijazi.

Mikoa itakayoathirika ni pamoja na Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Kanda ya Ziwa(Kagera, Mwanza, Geita, Mara na Shinyanga), Tanga, Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Kaskazini mwa mikoa ya Morogoro, Pwani na visiwa vya Mafia Zanzibar.

Pia alisema mvua hizo zinaweza kuleta madhara kwenye sekta ya kilimo, miundombinu na usafirishaji ambapo uharibifu unaweza kutokea kwenye maeneo hayo lakini pia inaweza kuleta faida kwenye sekta ya nishati kwa kuongezeka kina cha maji kwenye mabwawa na wakulima watakao lima mazao yanayostahimili mvua kubwa.

 

error: Content is protected !!