Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema tayari makubaliano nane yamefikiwa kati ya Tanzania na Urusi ikiwa ni sehemu ya matunda ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini humo.
Akizungumza jana Juni 7, jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), kwenye mkutano na wahariri pamoja na wanahabari, Prof Mkumbo amesema miongoni mwa makubaliano hayo ni Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuanza kufundisha Lugha ya Kirusi, huku vyuo vinne nchini Urusi vikiendelea kufundisha Lugha ya Kiswahili.
Amesema pia hati ya makubaliano ya elimu kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania na ile ya Urusi itasaidia kutambuliwa kwa tuzo na vyeti vya vyuo vya pande zote mbili, sambamba na upatikanaji wa ufadhili wa nafasi 150 za Watanzania kwenda kusoma nchini Urusi.
Pia, Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT) kitapokea walimu kutoka Urusi watakaokuja kufundisha masuala ya Akili Unde (AI), hatua inayolenga kuimarisha ujuzi wa teknolojia za kisasa nchini.


