Mama amuua binti yake

HomeKitaifa

Mama amuua binti yake

Mama na mwanaye wa kiume wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kumuua binti wa kumzaa wa mama huyo.

Washitakiwa hao ni Sofia Mwenda(61), Mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam na Alphonce Magombola(34) mkazi wa Bunju B ambao wamefikishwa mahakamani hapo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ritta Tarimo.

Wakili wa Serikali Faraji Ngukah, amedai tukio hilo lilitokea Desemba Mosi mwaka 2020 eneo la Kijichi wilayani Temeke, Dar es Salaam ambapo washitakiwa hao walishirikiana kumuua Beatrice Magombola.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa hawakurusiwa kujibu lolote kwa sababu mahakamani hiyo, haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji

Upande wa mashitaka umedai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kabla ya Hakimu kutoa tarehe, mshitakiwa Magombola, alinyoosha mkono na kudai kuwa alikamatwa na polisi tangu Machi 17, mwaka huu kisha akapelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

Magombola amedai baada ya kufikishwa kituoni hapo alipata mateso makubwa hadi kusababisha mguu wake kuumizwa hivyo aliomba kupatiwa matibabu.

Hakimu Ritta baada ya kusikiliza hoja hiyo, amesema kuwa mahabusu ya serikali kuna hospitali ambapo watuhumiwa wanapatiwa matibabu na kama wakishindwa anapelekwa sehemu nyingine.

Pia mshitakiwa wa pili ambaye ni mama mzazi wa Magombola, amedai kuwa alikamatwa Aprili 18 mwaka huu na jana ilikuwa siku yake ya kwenda kliniki ya macho kwani anasumbuliwa na macho.

Amedai baada ya kukamatwa alipelekwa Kituo cha polisi Mabatini ambapo alikaa siku tatu na baada ya muda alihamishiwa Kituo cha Polisi Oysterbay, ambako alipigwa sana na kusababisha kuumwa na nyonga.

”Nilipigwa hadi mkono na mguu unanisumbua sana naomba kupata matibabu,” amedai.

Wakili Ngukah, amedai kuwa kwa kawaida mahabusu zina hospitali kwa ajili ya watuhumiwa, hivyo atapatiwa matibabu.

Hakimu Ritta ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 28, mwaka huu kwa kutajwa na washitakiwa walirudishwa rumande.

error: Content is protected !!