Zungu awashangaa wanaolalamika tozo za miamala ya simu

HomeKitaifa

Zungu awashangaa wanaolalamika tozo za miamala ya simu

Naibu Spika Mussa Azzan Zungu amewashangaa baadhi ya wananchi wanaolalamikia tozo za miamala ya simu na benki na kuachwa kuzungumzia fedha wanazokatwa na makampuni ya simu wanapotoa au kutuma pesa.

Amesema makato ya makampuni hayo ni makubwa kuliko tozo ya Serikali.

“Jana Serikali imetangaza kupunguza gharama za miaamala, lakini wananchi wengi wanalalamikia kodi ya Serikali, hawatazami mapato yanayokatwa na mabenki na makampuni ya simu,” amesema Zungu leo Septemba 21, 2022 Bungeni jijini Dodoma.

Naibu Spika Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Iala amehoji kwa nini Serikali “ipigwe madongo” kwa tozo ambazo zinatumika kuboresha huduma za kijamii na kuacha hoja ya fedha wanazotozwa wananchi wakati wanafanya miamala ya fedha kwa njia za kielektroniki ikiwemo simu.

“Lazima hii iwe regulated (isimamiwe), benki unatuma pesa wanachukua pesa nyingi zaidi ya Serikali, lakini Serikali inayojenga madarasa na vituo vya afya ndiyo inalaumiwa.

“Kwa hiyo kuna ki-syndicate (mtandao) kinatengenezwa kuipiga dongo Serikali wakati pesa wanachukua watu wengine, hili litazamwe ni namna gani mta regulate (mtasimamia) mapato ya benki kupunguza gharama za service charge (huduma) zao pamoja na gharama za simu,” amesema Zungu wakati akihitimisha kipindi cha maswali na majibu.

Amesema mchanganuo wa makato wakati wa kutoa au kutuma pesa kwa njia ya simu yanaonyeshwa kabla mtu hajakamilisha muamala, “utaona makato ya Serikali yapo chini sana na mapato wanayochukua makampuni ya simu na taasisi za kifedha yapo juu zaidi.”

 

error: Content is protected !!