Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Nchini Switzerland katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Balozi Mulamula ameuhakikisha ujumbe wa wafayabiashara hao kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ni salama na hivyo wasisite kuwekeza.
“Serikali imejitahidi sana kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hivyo nawasihi kutumia fursa hiyo kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo, kilimo, nishati, madini na nyinginezo,” alisema Balozi Mulamula.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya ‘Global Network’, Bw. Stefan Barny emeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa maboresho makubwa katika sekta ya biashara na uwekezaji.
“Mazingira ya biashara hapa Tanzania nilikuwa nayasikia tu, ila baada ya kuja na kuonana pamoja na kujadiliana na wadau wa sekta za biashara na uwekezaji tumeridhishwa na mazingira ya biashara hapa Tanzania,” alisema Bw. Barny.
Bw. Barny ameongeza kuwa atawashawishi wafanyabiashara wenzake kutoka Uswisi kuja kuwekeza Tanzania kwan fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana Tanzania ni nyingi.
“Tumepanga kuwekeza katika sekta ya kilimo hasa katika sekta za kilimo hasa katika usindikaji wa mazao ya chakula, biashara na uwekezaji, madini na nishati….tumepanga kufungua kiwanda rasmi hapa Tanzania mwakani,” aliongeza Bw. Barny.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Balozi wa Switzerland hapa Nchini, Mhe. Didier Chassot, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.