Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu na Mjumbe wa kamati Kuu ya Chama hicho, Godbless Lema wametangaza kuwa watarejea nchini hivi karibuni ili kuendeleza jitihada za kudai Katiba mpya.
Wakizungumza katika kongamano la Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) mkoa Arusha leo Mei 21, 2022 wamesema siku ya kurejea itatangazwa na watapokewa kwa uwazi.
Akizungumza kupitia mtandao, Lissu amesema wamekuwa wakiahidi kurejea nchini mara kadhaa lakini kuna vitu vichache bado havijakaa vizuri.
“Lazima tutarejea nchini, tumekuwa tukiahidi kurudi lakini kuna vitu vidogo kuhusiana na masuala ya usalama wetu ila tutakuja tumechoka kukaa ugenini” amesema Lissu
Amesema siku ya kurejea nchini itatangazwa na watakuwa na mkutano na wananchi na wakifika wataendelea na kazi ya kuimarisha nchama kupitia mikutano ya hadhara na Katiba mpya.
“Mimi na Lema tutarudi pia Wenje na wengine kwa sababu mnajua mazingira tuliyoondokea nchini”amesema
Hata hivyo Lissu amewataka vijana wa Chadema kutambua kuwa bado sheria nyingi zilizopitishwa na utawala wa Serikali ya awamu ya tano hazikafutwa.
“Sheria kandamizi bado zipo ila sasa Rais Samia anajitahidi kurejesha mahusiano lakini hatuwezi kujihakikishia usalama wa kufanya siasa bila kuendelea kuzungumza”amesema
Amesema anaunga mkono jitihada ambazo anafanya Rais Samia Suluhu Hasaan kuanza mazungumzo na viongozi wa chadema ili kurejesha mahusiano mazuri katika Taifa.
chanzo: Mwananchi