Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka Watanzania wajikinge na ugonjwa wa Covid-19 kwa kuwa kuna dalili za kuingia kwa wimbi la tano la virusi vya corona.
Ummy alisema wimbi hilo limeripotiwa katika nchi za Kenya na Afrika Kusini huku akieleza kwamba kazi ya utoaji chanjo nchi inakabiliwa na changamoto ya wananchi kutotimiza dozi.
“Tumebaini kuwa baadhi ya walengwa waliopata dozi ya kwanza ya chanjo zinazotolewa kwa dozi mbili hawarudi kupata dozi ya pili. Mathalani , kwa kipindi cha mwezi Februari, 2022 wateja ambao hawakurdui kupata dozi ya pili ya chanjo aina ya Sinopharm ni 308,164 sawa na asilimia 25 ya wateja wote waliopata chanjo,” alisema Ummy.
Aidha, Waziri Ummy alisema chanjo ni hiari, hakuna haja ya kulazimisha wananchi kuipata chanjo hivyo wauguzi na madaktari wasiwanyime wananchi huduma kwa sababu ya kutochanja.