Iwapo una ndoto ya kumiliki nyumba lakini hauna fedha, huenda ukapata mikopo ya kujengea nyumba kutoka benki za biashara Tanzania licha ya kuwa katika baadhi ya taasisi hizo za kifedha utakutana na riba kubwa jambo ambalo ni kikwazo kwa watu wenye kipato kidogo.
Hadi Mei 15, 2022 kwa mujibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,kulikuwa na benki 32 za Tanzania zilitoa mikopo ya nyumba kwa wananchi 6,177 yenye thamani ya Sh496.6 bilioni.
Ni benki gani ambazo zinatoa mkopo wa nyumba?
Mikopo hiyo, takwimu za wizara zinabainisha kuwa ilitolewa na benki hizo chini ya uwezeshaji ya Kampuni ya Mikopo ya Nyumba ya Tanzania (TMRC) na sehemu kubwa ya mikopo ilitolewa na benki tano za CRDB, Stanbic, Azania, NMB na Benki ya Taifa ya Biashara Afrika (NCBA).
Benki hizo tano kwa pamoja zinamiliki theluthi mbili au asilimia 66.6 ya soko lote la mikopo ya nyumba Tanzania kwa mwaka 2021/22 unaoisha Juni 30.
CRDB ndiyo kinara wa utoaji wa mikopo hiyo ambapo kwa mujibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa mikopo ya nyumba kwa watu 1,653 ikiwa na thamani ya Sh194.3 bilioni.
Kwa mikopo hiyo, CRDB inamiliki soko la mikopo ya nyumba kwa asilimia 39.1 ikiwa katika nafasi ya kwanza Tanzania.
Benki hiyo ya biashara ambayo ni moja ya benki zenye matawi mengi nchini imefuatiwa kwa mbali na benki Stanbic ambayo ilitoa mikopo yenye thamani ya Sh45.9 bilioni kwa wananchi 217 huku ikichuana vikali na Azania ambayo imeshika nafasi ya tatu ikifuatiwa na NMB katika nafasi ya tano ambayo ilitoa mikopo yenye thamani ya Sh30.9 bilioni kwa wananchi 312.
Tano bora ya benki zinazoongoza kutoa mikopo ya nyumba imefungwa na NCBA ambayo ilitoa mikopo kwa wananchi 134 yenye thamani ya Sh24.3 bilioni.
Viwango vya riba vya mikopo ya nyumba hutofautiana kutoka benki moja hadi nyingine kutegemeana na kiwango cha mkopo kinachoombwa na muda ambao mtu anatumia kulipa mkopo husika.
Kuongezeka kwa ushindani wa taasisi za fedha zinazotoa mikopo hiyo kumesaidia kushusha riba kutoka asilimia 22 iliyokuwa inatumika mwaka 2009 hadi asilimia 15 na asilimia 19 mwaka 2021.
source: Nukta Habari