Benki ya Dunia imeipongeza Tanzania kwa kuamua kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye maeneo ya uzalishaji kikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi mambo ambayo yatachochea ukuaji wa kipato cha wananchi na kukuza uchumi wa nchi.
Pongezi hizo zimetolewa Jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Kusini Mashariki, Bi. Victoria Kwakwa, alipokutana na kufanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Aliahidi kuwa Benki yake na washirika wake wengine watasaidia juhudi za Serikali za kufanikisha mapinduzi katika sekta hizo muhimu kwa kutoa fedha pamoja na ushauri wa kitaalam ili mpango huo wa kuendeleza kilimo, mifugo na uvuvi uwe na tija.
Bi. Kwakwa alisema kuwa changamoto ya UVIKO 19 na vita vinavyoendelea baina ya Urusi na Ukraine vimeibua changamoto kubwa ya uhaba wa mazao ya nafaka na kwamba Tanzania ikijipanga vizuri inaweza kuwa ghala la chakula na kuifanya ijitosheleze kwa chakula na kutoagiza chakula kutoka nje.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa Serikali imeamua kuwekeza fedha kwenye maeneo ya uzalishaji akitolea mfano wa ongezeko la bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 200 hadi zaidi ya shilingi bilioni 900 ili kuiwezesha sekta hiyo kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuzalisha ajira kwa wananchi.
Dkt. Nchemba aliishukuru Benki hiyo kwa uwekezaji wa dola za Marekani bilioni 2.8 katika miradi 11 ya kimkakati iliyowasilishwa katika Benki hiyo katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kuwa uwekezaji huo utaisaidia nchi kupambana na umasikini pamoja na ukuaji jumuishi wa maendeleo ya watu na kuahidi kuwa fedha zinazopatikana kutoka katika Benki hiyo zinatumika ipasavyo ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Aidha, Dkt. Nchemba, aliishukuru Benki hiyo kwa kuiidhinishia Tanzania kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia mpango mpya wa utoaji mikopo na misaada wa IDA 20 ulioanza kutekelezwa rasmi mwezi Julai, 2022.
Aliiomba Benki hiyo kuharakisha utoaji wa fedha ili miradi iliyopangwa kutekelezwa kupitia mpango huo wa miaka mitatu iweze kutekelezwa na kwamba Serikali itashukuru endapo kiwango hicho cha fedha kitaongezwa ili miradi iliyopo hivi sasa inayokadiriwa kugharimu dola za Marekani bilioni 4.9 iweze kukamilika kwa wakati.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha na Mipamgo, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamisi Shaaban, Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Rished Mohamed Bade na Viongozi wengine kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.