Serikali ya Urusi imesema sera ya uwazi ya Rais Samia Suluhu Hassan inawatia moyo na kuahidi kuhamasisha uwekezaji,biashara na watalii wengi wa Urusi kuja Tanzania.
Balozi wa Urusi nchini, Andrew Avestisyna alisema hayo ofisini kwake Dar es Salaam wakati wa mahojiano na waandishi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).
Balozi Avestisyna alisema kwa kuwa katika miaka ya 1960 uhusiano wa Urusi na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania ulijikita zaidi kwenye masuala ya kisiasa ikiwemo harakati za kupigania uhuru, kwa sasa Urusi inaona vyema kupanua uhusiano huo katika masuala ya uchumi, biashara na uwekezaji.
“Moja ya vipaumbele vyangu kama Balozi hapa ni kuhamasisha watalii, wawekezaji na wafanyabiashara wa Urusi kuja Tanzania. Mwezi Januari hadi Machi mwaka 2020, watalii takribani 82,000 wa Urusi walitembelea Zanzibar,” alisema Balozi Avistesyna.
Alisema baadaye idadi hiyo ya watalii ilipungua kutokana na Covid-19 japo kwa sasa wameanza tena kuja taratibu, ila anatumaini wataongezeka.