Mradi wa Sh270 bilioni watua wanakijiji ndoo

HomeKitaifa

Mradi wa Sh270 bilioni watua wanakijiji ndoo

Zaidi ya wakazi 10, 000 wa Kijiji cha Bugayambelele Kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga, wameondokana na adha ya kukosa huduma ya maji baada ya mradi wa maji ya Ziwa Victoria wa  Sh270 bilioni kukamilika.

Mradi huo unatekelezwa na mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (Shuwasa) ambao umeondoa changamoto ya wananchi kufuata maji umbali wa kilomita tano.

Wakizungumza leo Julai 31, 2023 baadhi ya wakazi wa kijiji hicho akiwemo Anna Chambi amesema walikuwa wanachota maji kwenye mito na madimbwi ambayo hujaa maji wakati wa masika huku ndoo ya lita 20 wakinunua kwa Sh500.

“Tulikuwa tunafuata maji kwenye mito ambayo nayo ikifika mwezi wa nane inakauka tunaanza kununua maji dumu Sh500 kwa kweli hali ilikuwa mbaya lakini leo hii tunaishukuru Serikali imetuona na kuondoa tatizo la maji Bugayambelele,” amesema Chambi

Mkazi mwingine wa kijiji cha Bugayambelele, Vedastina Nyakonga amesema kabla ya kupata huduma ya maji ndoa zao zilikuwa hatarini kwani walikuwa wanalazimika kuamka saa tisa usiku kwenda kuwahi kupanga foleni ya kusubiri maji na kuwaacha waume zao wamelaa.

“Kweli Rasi Samia Suluhu Hassan amemtua mama ndoo kichwani tulikuwa tunateseka tunatoka nyumbani usiku saa tisa na watoto wale ambao ni wakubwa nyumbani anabaki baba yao na watoto wale wadogo halafu njiani tunakutana na fisi lakini Mungu anatulinda,” amesema Vedastina

Mwenyekiti wa kitongoji cha Bugayambelele, Jacob Peter amesema upatikanaji wa maji ilikuwa ni kilio kwa Kaya 332 zenye watu 1,100.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Kaimu Mkurugenzi (Shuwasa), Sara Emmanuel amesema mradi huo wa maji safi na salama kutoka mtandao wa maji ziwa Victoria utawanufaisha wakazi zaidi ya 10,000.

Amesema mradi huo wa maji utaondoa adha waliyokuwa wakipata wananchi kutembea umbali mrefu ambapo kwa sasa kilio chao kimepatiwa ufumbuzi na kumtua mama ndoo kichwani na kubainisha kuwa hatua inayofuata sasa ni kuunganisha huduma ya maji majumbani.

SOURCE| MWANANCHI NEWSPAPER

error: Content is protected !!