Serikali kuajiri walimu 42,697 mwaka 2022-23

HomeUncategorized

Serikali kuajiri walimu 42,697 mwaka 2022-23

Huenda uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hesabu ukapungua nchini Tanzania na kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika masomo hayo mara baada ya Serikali kusema iko mbioni kuajiri walimu 42,697.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Juma Kipanga aliyekuwa akizungumza bungeni jijini Dodoma Septemba 22, 2022 amewaambia Wabunge kuwa tayari kimeshaombwa kibali cha kuajiri walimu zaidi ya 42,697 na kipaumbele kitakuwa kwa walimu wa Sayansi na Hesabu.

“Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) katika mwaka huu wa fedha  imeshaomba kibali cha kuajiri walimu 42,697 kipaumbele kitakuwa walimu wa masomo ya Sayansi, Hisabati na wanaojitolea,” amesema Kipanga.

Naibu Kipanga ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Esther Matiko aliyehoji kwanini Serikali haijaweka mkakati wa kuajiri walimu wa Sayansi na Hisabati ikiwa ni asilimia 33 tu ya wahitimu wa masomo hayo walioajiriwa.

Kwa mujibu wa Kipanga kati ya mwaka 2015 hadi 2022 jumla ya wahitimu 33,492 wa kada ya ualimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati wamehitimu katika vyuo mbalimbali huku wahitimu 13,383 ndiyo walioajiriwa na Serikali.

Shule za Serikali nchini Tanzania zimekuwa zikikabiliwa na uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati jambo linalosababisha ufaulu katika masomo hayo kuwa mdogo.

Itakumbukwa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yaliyotangazwa mwezi Mei mwaka huu na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) ni wanafunzi watatu pekee kutoka shule ya Serikali walioingia katika orodha ya wanafunzi kumi bora waliofanya vizuri kwenye masomo ya Sayansi.

Huenda mpango huo wa Serikali kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ukasaidia shule zake kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa.

error: Content is protected !!