Rais Samia Suluhu Hassani jana Oktoba 17,2022 amezima umeme uliokuwa unatumia jenereta na kuwasha umeme wa gridi ya Taifa na kuwataka wananchi kutunza miundombinu ya umeme iliyowekwa katika maeneo yao.
Akizungumza katika ziara yake ya siku ya pili, akiwa wilayani Kasulu mkoani Kigoma, Rais Samia amesema wananchi wamepata umeme wa kutosha utakaowasaidia kufanya shughuli zao za kimaendeleo.
Rais Samia amewataka wakazi wa Kasulu kulinda majenereta yaliyokuwa yakitumika awali, kwani yatatumika wakati wa dharura na kulinda miundombinu ya umeme iliyopo njiani inayofikisha umeme wilayani humo.
“Pamoja na kwamba tumezima jenereta zilizokuwa zinatumika lakini tumeweka akiba na nawaomba jenereta hizi ni mali yenu watu wa Kasulu, pamoja na kwamba yanatunzwa na shirika la umeme (Tanesco), ni muhimu kuyatunza yasiharibiwe na kituo hiki kibaki kama kilivyo,” amesema Rais Samia.
Amesema maendeleo hayo ni kwa ajili yao na serikali inafanya kwao na wanafanya kwasababu wananchi waweze kufanya shughuli zao za kila siku za kimaendeleo katika wilaya yao hivyo waweze kulinda mali zilizopo kwa manufaa yao.
Amesema mkoa wa Kigoma upo pembezoni mwa nchi ya Tanzania wamepeleka umeme wa uhakika ili wawekezaji waweze kwenda kwa wingi na kuwekeza katika mkoa huo, kama ni dhahabu ziweze kuchenjuliwa na wawekezaji kutoka nchi jirani.
Naye Waziri wa Nishati, January Makamba amesema umeme huo utasaidia kuondoa gharama nyingi za uendeshaji, matengenezo na mafuta.
“Umeme wa gridi kufika kigoma kuna manufaa makubwa sana ya kiuchumi, Mkoa wa Kigoma kwa vituo vyetu hivi vya kuzalisha umeme kwa majenereta ni megawati 14 lakini umeme uliokuja kwa gridi sasa hivi ni wa megawati 20.” amesema Waziri Janauary.
Amesema kwa mwaka mafuta peke yake kwenye vituo vya kuzalisha umeme kwenye jenereta ni Sh52 bilioni kwa mwaka lakini mapato yanayopatikana ni Sh14 bilioni.
“Kwa hiyo Serikali ilikuwa inatoa ruzuku inatumia ela nyingi kuliko mapato tuliyokuwa tunayapata,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali mkoani hapo, kituo hicho kwa Kasulu pekee kimekuwa kikitumia Sh36 milioni kwa siku za mafuta, lita 12 kwa siku na kwa mkoa mzima mafuta yanatumika kwa Sh144 milioni kila siku.