Wananchi wa kijiji cha Namatumu Kata ya Malika Halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara, wamesema Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), wilayani Masasi mkoani Mtwara, amewaondolea keri ya miaka 50 bila maji.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana kijijini hapo katika hafla fupi ya uzinduzi wa mradi wa maji wenye thamani ya Sh. milioni 308 uliojengwa na RUWASA katika kijiji cha Namatumu, mjini Masasi.
Maimuna Saisi mkazi wa Kijiji hicho, alisema walitembea umbali mrefu mpaka vijiji vya kata ya jirani ya Mumbaka kwa ajili ya kutafuta huduma ya maji ambayo hayakuwepo.
Alisema kutokana na kukosekana kwa maji wanawake walilazimika kuamka usiku wa manane kutafuta maji hali iliyohatarisha ndoa zao na kwamba sasa zitaendelea kuimarika.
Bibie Matwani mkazi wa kijiji cha Namatumu alisema kutokana na adha ya upatikanaji wa maji wanawake wa kijiji hicho walikuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi kwa wakati mmoja huku wakitumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya kazi za kimaendeleo.
” Tunaipongeza serikali kwa kutuletea maji safi na salama na ile changamoto ya upatinakaji wa maji na salama katika kijiji chetu tumeondokana nayo kabisa kwa sasa na hii ni baada ya miaka zaidi ya 50 sasa hivi wananchi tunaipongeza serikali kwa hili,” alisema Bibie.