Ombi la watumishi la miaka 5 lajibiwa na Rais Samia

HomeKitaifa

Ombi la watumishi la miaka 5 lajibiwa na Rais Samia

July 13,2017 akiwa Waziri wa Utumishi wa Umma, Mhe. Angela Kairuki alisema hatima ya kulipwa mafao kwa watumishi waliokutwa na vyeti feki serikali itatolea tamko hivyo wawe wavumilivu.

Oktoba 26, 2022 ikiwa ni miaka mitano tangu serikali itoe ahadi hiyo, Rais Samia Suluhu ameridhia watumishi hao walioondolewa kwenye ajira zao kwa kuwa na vyeti bandia warejeshewe michango yao ya hifahdi ya jamii.

Watumishi hao waliondolewa kazini baada ya uhakiki wa vyeti uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), kati ya Oktoba 2016 hadi Aprili 2017.

Akizungumza kuhusu uamuzi huo jana jijini Dodoma, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alisema malipo hayo yataanza kulipwa kuanzia Novemba mosi.

“Rais Samia ameridhia watumishi wote walioondolewa kazini kwa kugushi vyeti warejeshewe michango waliyokatwa kwenye mishahara yao na kupelekwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii,” alisema.

Mmoja wa watumishi walioondolewa kazini, Emmanuel Manga alisema wanamshukuru Mungu na Rais Samia kwa kuwarejeshea michango yao.

“Ni uvumilivu tu umetufanya kufika hapa. Tunamshukuru mama (Rais Samia) kwa uamuzi huu kwa sababu ni miaka mitano sasa mtu uko benchi(hakuna kazi), si suala dogo na unakuta mtu ulikuwa na maisha yako lakini ndio hivyo tena,” alisema Emmanuel.

error: Content is protected !!