Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wanafunzi walionufaika na mikopo ya elimu ya juu kukumbuka kurudisha fedha hizo ili ziweke kunufaisha wanafunzi wengine.
Ameyasema hayo leo Februari 11, 2023 wakati akizungumza na Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) na Zanzibar (TAHLIFE) jijini Dodoma.
“Mnaonufaika na mikopo mkipata kazi rudisha ili mdogo wako na wewe apate mkopo na yeye asome, sasa mkisoma mkatoka mkaenda kujikausha sio wazalendo wala hamtendi haki,” amesema Rais Samia.
Pia, Rais Samia amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu kulinda na kuzingatia maadili huku wakiwafunza wadogo zao kufuata maadili mema na kulitunzia heshima taifa.
“Lindeni wadogo zenu vinginevyo mtakuja kuwa na taifa la ajabu, huko tunakotembea nje mambo sio swari, tuishini kwa mila na desturi zetu, mambo ya kuletewa yapo ya kuiga, suti zimetoka nje tunavaa tunapendeza, unataka kusema kizungu cha kubana pua sema, lakini yale mengine acha” amesema Rais Samia
Aidha katika hatua nyingine Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Elimu kuyatoa majengo yanayotumika na wizara hiyo kwa sasa kwenda TAHLISO mara tu wakatapohamia katika majengo mapya ya Wizara hiyo yanayojengwa Mtumba Jijini Dodoma
“Nitoe maelekezo kwa waziri wa elimu kwamba najua karibu mnamaliza majengo yenu pale Mtumba, kwahiyo mtakapohamia mtumba yale majengo mnayotumia sasa myakabishi kwa TAHLISO”
Rais Samia ameahidi kutoa samani na vitendea kazi vya ofisi za Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) na Zanzibar (TAHLIFE).