Rais Samia : Uongozi bora ni msingi wa maendeleo

HomeKitaifa

Rais Samia : Uongozi bora ni msingi wa maendeleo

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuna shida katika uongozi bora Tanzania, jambo ambalo limekuwa likiibua changomoto kwa baadhi ya viongozi wa Serikali wakiwemo mawaziri na manaibu mawaziri kutekeleza wajibu wa kikamilifu wa kuwatumikia Watanzania.

Amesema uongozi bora ni miongoni mwa misingi ya maendeleo iliyoasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere ikiwemo watu, siasa safi, pamoja na ardhi.

​Rais Samia aliyekuwa akifungua kikao kazi cha mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu jijini Arusha hii jana Machi 2, 2023, amewaambia wahudhuriaji dhumuni la kikao hicho ni kujadili kwa undani namna ya kumfanya kiongozi kuwa bora.

“Katika kujenga dhana ya uongozi bora, nimeamua tuwe na mkutano huu  ili tuzungumze na tuelekezane namna ya kujenga mustakabali wa maelewano katika kulitumikia Taifa letu, tutakumbushwa misingi ya uongozi na taratibu za utendaji kasi serikalini…,” amesema Rais Samia.

Kwa mujibu wa Rais Samia kutofanyika kwa mikutano kama hiyo kwa muda mrefu kumeleta athari zinazoonekana wazi katika utendaji Serikalini ambapo kuna ombwe la uelewa wa taratibu za utendaji kazi jambo linalosababisha  migongano isiyo ya lazima na kuathiri uwezo wa kuhudumia wananchi.

“Hii ni moja ya sababu ya viongozi kubadilishwa mara kwa mara ili kuiepusha Serikali na fedheha ya kuwa na viongozi wanaozifanya wizara kuwa sehemu ya malumbano na migawanyiko isiyo na tija,” amesema Rais Samia

Samia amesisitiza kwamba anatarajia mkutano huo utakuwa na matokeo yenye tija kwa viongozi hao kwa kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika kuhudumia wananchi na hatofurahi kama viongozi hao hawatotilia maanani umuhimu wa mkutano huo.

Maada kuu zitakazojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na taratibu za uendeshaji shughuli za Serikali, mahusiano na mipaka, utoaji wa maamuzi makubwa na sera ndani ya Serikali, usimamizi wa rasilimali watu, mahusiano ya Serikali na na sekta binafsi pamoja na miongozo ya utendaji kazi Serikalini.

Maada hizo zitagawanyika katika maada ndogo 17 ambazo zitawasilishwa na watoa maada walioteuliwa akiwemo Mizengo Pinda ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, Katibu Mkuu mstaafu pamoja na Palamagamba Kabudi ambaye ni mbobevu wa sheria na mshauri wa Rais.

error: Content is protected !!