Licha ya kupongeza hatua hiyo ya Serikali kuitikia wito na kuamua kuzivalia njuga changamoto zao Mwenyekiti wa wafanyabiashara sokoni hapo Martin Mbwana amewaomba wafanyabiashara kuitikia wito wa Serikali wa kufungua maduka yao.
“Kwa kuwa keshokutwa tunakaa kikao, naomba niwatangazie wafanyabiashara tukubali agizo la Waziri Mkuu tumuunge mkono, tufungue biashara zetu, tunaamini baada ya kikao kero zetu zote zitakuwa zimeisha,” amesema Mbwana huku akipigiwa makofi.
Sakata la mgomo wa wafanyabiashara limegonga vichwa vya vyombo vya habari hii leo na kusababisha baadhi ya Wabunge kuomba suala hilo lijadiliwe kwa dharura bungeni ambapo Spika Tulia Ackson aliomba muda ili ajiridhishe.
Baada ya juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla kuwashawishi wafanyabiashara hao kuendelea na shughuli zao kugonga mwamba, Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa taarifa kuwa itakutana na wafanyabiashara hao Mei 17, 2023 katika ofisi za Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo Waziri Majaliwa alifika na kuzungumza na viongozi wa wafanyabiashara kusikiliza kero zao na kisha kuelekea soko la Kariakoo ambako amezungumza na wafanyabiashara hao ana kwa ana na kuahidi kupokea changamoto nyingine Mei 17.