Mnamo tarehe 28 Februari, 2022, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (Tanzania Ports Authority [TPA]) iliingia Makubaliano ya Awali (Memorandum of Understanding [MoU]) na Kampuni ya DP World (DPW) inayomilikiwa na Serikali ya Dubai (the Emirate of Dubai).
Kwa mujibu wa mapendekezo ya kuridhia Mkataba huu yaliyowasilishwa na Serikali, kuridhiwa kwa Mkataba huu kutakuwa na manufaa yafuatayo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania:
a. Kuongeza fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutokana na uwekezaji mkubwa na ongezeko la shehena ya mizigo itakayopitia bandari ya Dar es Salaam.
b. Kuongezeka kwa ufanisi katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi na kuleta tija stahiki katika mnyororo wa thamani wa huduma za bandarini nchini.
c. Kuongezeka kwa pato la taifa kutokana na uboreshaji wa shughuli za kibandari.
d. Kuongezeka tija na kuwezesha mwendelezo wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo imekuwa ikijengwa na Serikali kama vile:
(i) Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge Railway-SGR),
(ii) ujenzi wa meli za mizigo katika maziwa makuu, na
(iii) Mradi wa Lango la Bahari la Bandari ya Dar es Salaam (Dar es Salaam Maritime Gateway Project- DMGP).
e. Kuchagiza na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi (multiple effect) zikiwemo kilimo, utalii, viwanda, mifugo, uvuvi, biashara na usafirishaji na hivyo kuboresha ustawi wa Watanzania kwa ujumla.
Kwa mujibu wa taarifa kwenye tovuti ya DP World1 , Kampuni hii imewekeza kwenye miundombinu ya bandari mbalimbali duniani (ports and terminals), huduma za meli (marine services), maeneo maalum ya kiuchumi (economic zones), maeneo ya maegesho na utunzaji mizigo (logistics) na maeneo ya kanda za kibiashara (trade corridors). Kampuni ina uzoefu wa zaidi ya miaka 20 ikiendeleza na kufanya maboresho ya miundombinu ya bandari barani Afrika.