Tanzania imeongeza idadi ya watalii wa kigeni wanaoingia nchini kwa asilimia 19 kufikia Septemba mwaka huu ikilinganishwa na idadi ya juu iliyopata kufikiwa ambayo ni kabla ya janga la Uviko-19 mwaka 2019, inabainisha ripoti iliyotolewa Novemba 30 mwaka huu ya Shirika la Umoja wa Mtaifa la Utalii Duniani (UNWTO) jijini hapa.
Ripoti hiyo iitwayo “World Tourism Barometer” toleo la Novemba, 2023, imebainisha kuwa kwa ukuaji huo, Tanzania inashika nafasi ya pili Afrika ikitanguliwa na Ethiopia ambayo utalii wake umekua kwa asilimia 26.
Kwa takwimu hizo Tanzania imeshika nafasi ya pili Afrika na ya 10 duniani ikiwa nyuma ya mataifa yaliyowekeza sana kutangaza utalii kwa njia mbalimbali ambapo Qatar imeongoza ikifuatiwa na Saudi Arabia, Andora, Albania huku mataifa mengi makubwa duniani yakionekana bado yanahaha kurejea katika takwimu za kabla ya Uviko.
Aidha, katika kipengele cha mapato ya sekta ya Utalii, Tanzania imekuwa ya 10 duniani na ya tatu Afrika (ikiwa nyuma ya Mauritius na Morocco kwa Afrika) katika nchi ambazo zimeongeza kwa kiwango kikubwa mapato yake ikilinganishwa na mwaka 2019 ambapo ripoti hiyo inaonesha kwa Tanzania yameongezeka kwa asilimia 26.
Mafanikio haya ni matokeo na ushahidi mwingine wa wazi wa juhudi kubwa za Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kazi nzuri ya wadau wa utalii.
Rais Samia binafsi ameshiriki filamu mbili za kuitangaza nchi yake ambapo filamu ya “Tanzania: The Royal Tour,” iliyoshirikisha watayarishani kutoka Marekani tayari imekuwa kivutio duniani huku ikielezwa pia nchi hiyo na Rais mwenyewe tena ameshiriki filamu nyingine ya “Tanzania: The Presidential Tour,” ikiandaliwa na magwiji kutoka nchini China.