Rais Samia Suluhu Hassan atasafiri kwenda Nchini Ufaransa kuhudhuria na kuwa Mwenyekiti mwenza wa mkutano wa kimataifa wa nishati safi ya kupikia unaowakutanisha Wakuu wa Nchi mbalimbali duniani.
Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi January Makamba leo Jijini Dar es salaam, amesema Rais Samia atakuwa Nchini Ufaransa kwa siku nne kuanzia May 12 hadi May 15 ambapo Tanzania imeshirikishwa kwenye mkutano huo kutokana na jitihada kubwa zinazofanyika ndani ya Tanzania kusukuma ajenda hiyo ya kuwawezesha Watu wote kutumia nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao na kulinda mazingira.
“Mkutano huo una malengo matatu, kwanza kuifanya hii iwe ajenda ya kimataifa na ipate Wadau wengi zaidi, pili ni kuchukua hatua madhubuti za kisera zinazoweza kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, na tatu ni Washiriki Nchi zilizoendelea na Taasisi za Fedha za kimataifa kutoa ahadi za fedha na misaada na Nchi kutoa ahadi za kubadilisha sera na sheria ili kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akiwa Ufaransa, Dr. Samia anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Ikulu jijini Paris katika kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Nchi hizo mbili.