Rais .Samia Suluhu Hassan amekabidhi boti 35 za kisasa kwa wavuvi wa Mkoa wa Tanga, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa ukopeshaji wa boti kwa wavuvi nchini.
Mradi huu, unaosimamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, unalenga kusaidia wavuvi katika Ukanda wa Pwani, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa ili kuongeza tija katika sekta ya uvuvi na kuhakikisha uvuvi endelevu.
Awamu ya kwanza ya mradi huu ilianza mwaka wa fedha 2022/2023 kwa gharama ya shilingi bilioni 11.5, ambapo boti 160 zilikopeshwa kwa wanufaika 3,163.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu Kijaji, amesema kuwa boti hizo zitasaidia si tu kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi, bali pia kudhibiti uvuvi haramu.
Ameeleza kuwa vijana 113 kutoka Mkoa wa Tanga, ambao hapo awali walijihusisha na uvuvi haramu, wameamua kubadili maisha yao na sasa wanajiunga na vikundi vya uvuvi halali kupitia mpango huo wa mikopo nafuu.