Fahamu kompyuta 5 bora za kununua

HomeElimu

Fahamu kompyuta 5 bora za kununua

Katika ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia matumizi ya kompyuta mpakato katika shughuli za masomo, biashara au kiofisi yameongezeka kwa kiasi kikubwa.

Inawezekana ukawa na mpango wa kununua kompyuta mpakato ili ikusaidie katika mojawapo ya shughuli tajwa hapo juu lakini unapata kigugumizi ni kompyuta ipi inakufaa kutokana na shughuli unayotaka kufanya.

Jarida la habari za teknolojia la nchini Marekani la C-NET limetaja orodha ya kompyuta mpakato tano bora kwa mwaka 2022 kwa kuzingatia gharama, kampuni iliyotengeneza, utendaji wake wa kazi pamoja na muonekano wake.

1: Apple MacBook Air M2 

Hii ndio kompyuta bora zaidi kwa mwaka 2022, ikiwa na muundo mpya wa inchi 13.6 kutoka inchi 13.3 ya mwaka uliopita. Imewekewa chipu ya M2 inayoiwezesha kompyuta hii kufanya kazi kwa kasi zaidi.

Ina kamera iliyoboreshwa zaidi hadi megapikseli 1,080 pamoja na betri yenye  uwezo wa kukaa na chaji kwa zaidi ya saa 18.

Itakulazimu kuwa na Sh2.8 milioni au Dola za Marekani 1,199 za marekani ili uweze kununua toleo hili la mwaka 2022.

: Acer Swift 3

Namba mbili ni kompyuta ya Acer Siwft 3 kutoka kampuni ya Acer. Ni kompyuta nyepesi ambayo ina uzito wa takribani kilogram 1.2 tu, skrini yake ina ukubwa wa inchi 14.

Kompyuta hii inapatikana katika vichakata vya aina mbili yaani Intel core au AMD ryzen. Hii ni mifumo ya uendeshaji ambayo huchangia kasi ya utendaji kazi wa kompyuta husika.

Betri yake ina uwezo wa kukaa saa saba mpaka 16 na kicharazio chake huwaka taa.

Ili kuipata kompyuta hii andaa kitita cha Sh2.3 milioni kwa toleo jipya la kizazi cha 12 au Sh1.6 milioni kwa toleo la mwaka 2021.

3: Dell XPS 13

Hii ni kompyuta mpakato inayozalishwa na Kampuni ya Teknolojia ya Dell ya nchini Marekani ambayo ilianzishwa mwaka 1984.

Kompyuta hii imefanyiwa marekebisho kadhaa kutoka ile ya mwaka 2020 ikiweMo kupunguzwa ukubwa na kuongezwa upana wa skrini yake hadi inchi 13.4 pamoja na kuiongezea uwezo na kasi ya  kuchakata vitu.

Ina nafasi ya gegabaiti 512 za kutunza kumbukumbu pamoja na gegabaiti nane kwenye mfumo wa kuchakata na kamera yake imeboreshwa hadi pikseli 720.

Ukiwa na Dola 999 za Marekani au Sh2.3 za Tanzania unaweza kununua toleo la mwisho kabisa la kompyuta hiyo.

4 : HP Pavilion Aero 13

Kama unatafuta kompyuta bora yenye kasi ya utendaji wa kazi ambayo inauzwa chini ya Dola 1000 za Marekani yaani Sh 2.3 milioni za Tanzania basi Hp Pavilion Aero 13 inakufaa.

Hii ni kwa sababu kompyuta hii inatumia kichakata cha AMD ryzen 7 inayoongeza kasi katika mifumo endeshi ya kompyuta.

Kompyuta hii ni nyepesi sana ikiwa na uzito wa paundi 2.2 ambazo ni sawa na gram 997.9. ina skrini yenye ukubwa wa inchi 13.3 pamoja na kamera yenye pikseli 720.

Hata hivyo kutokana na wembamba wake huenda baadhi ya watu wasifurahishwe na udogo wa sehemu ya kicharazio pamoja na kukosekana kwa sehemu ya kuweka kadi ya MicroSD.

Utaipata endapo tu mfukoni mwako utakuwa na fedha kuanzia Sh1.2 milioni.

5: Lenovo Yoga 7i 

Kompyuta namba tano ni kutoka kampuni ya Lenovo ambayo imepewa jina la yoga kutokana na skrini yake kuwa na uwezo wa kuzunguka kwenye nyuzi 360.

Ni miongoni mwa kompyuta nyepesi inayofaa kwa kazi za ofisini au shuleni ambapo skrini yake ina ukubwa wa inchi 14 pamoja na betri yenye uwezo wa kukaa na chaji kwa saa 13.

Ina sifa za ziada za ulinzi ikiwemo kamera ya tovuti pamoja na uwezo wa kutambua alama za vidole pamoja na skrini inayoshikika (touch screen)

Kompyuta hii ni toleo la 11 la intel core ambayo inapatikana kuanzia Sh2.7 milioni sawa na Dola 1169 za Marekani.

SOURCE: NUKTA

error: Content is protected !!