Benki ya Dunia yaitengea Tanzania trilioni 5

HomeKitaifa

Benki ya Dunia yaitengea Tanzania trilioni 5

Benki ya Dunia imeshukuriwa kwa kuitengea Tanzania dola za Marekani bilioni 2.1 sawa na shilingi trilioni 4.9 katika mzunguko wa 20 wa IDA (Julai 2022- Juni 2025) kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba alitoa shukurani hizo wakati akizungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na KUsini mwa Afrika, Victoria Kwakwa wakati wa Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayoendelea Washington DC, Marekani.

Kati ya kiasi hicho, dola za Marekani milioni 535 sawa na asilimia ishirini na tano ya mgao tayari zimeshaidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Dunia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini (dola za Marekani milioni 335); na uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi (dola za Marekani milioni 200).

Aidha, Kwakwa aliipongeza Tanzania kwa hatu inazochukua kusimamia uchumi na maendeleo ya wananchi na kuahidi kuyafanyia kazi maombi ya Tanzania kusaidia ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR na atawaelekeza wataalamu kupitia nyaraka za mradi huo.

error: Content is protected !!