Mapato ya utalii yazidi kupaa

HomeKitaifa

Mapato ya utalii yazidi kupaa

Mapato yanayotokana na utalii yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 714.59 kwa mwaka 2020 hadi kufikia Dola za Kimarekani milioni 1,310.34 (zaidi ya Sh trilioni 3.05 mwaka 2021.

Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa Septemba 30, 2022 Jijini Arusha na Mwenyekiti wa Kamati ya Ripoti ya Utafiti wa Watalii ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma S. Mkomi imeonyesha.

Naibu Katibu Mkuu Mkomi amesema taarifa ya utafiti huo inaonesha kuwa Tanzania inazidi kufanya vizuri katika sekta ya utalii huku mapato yatokanayo na utalii yakiongezeka mwaka hadi mwaka.

Amesema mwaka mmoja baada ya mlipuko wa janga la UVIKO-19, idadi ya watalii iliongezeka kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 hadi kufikia watalii 922,692 mwaka 2021 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 48.6.

Amezitaja sababu zilizochangia ongezeko la watalii hapa nchini mara baada ya mlipuko wa Janga la UVIKO 19 kuwa ni jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na Sekta binafsi katika kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi.

Mkomi amesema, matokeo ya utafiti yanaonesha idadi kubwa ya watalii walikuja hapa nchini kwa ajili ya kutembelea hifadhi za wanyamapori na fukwe.

Utafiti huo umefanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Benki Kuu Tanzania (BOT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Idara ya Uhamiaji, Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Shirikisho la wawekezaji katika Sekta ya Utalii Zanzibar ( ZATI).

Mkomi amesema takwinu za utafiti huo, zimepatikana kutokana na utafiti uliofanywa katika vituo vikubwa nane vya watalii, ikiwemo viwanja vya ndege vya kimataifa pamoja na maeneo ya njia za kuingilia na kutokea watalii.

Matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa idadi kubwa ya watalii wametokea nchi ya Ufaransa ikifuatiwa na Marekani, Kenya pamoja na Zambia.

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu Mkomi amesema matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku hapa nchini yaliongezeka kutoka dola za Kimarekani 152 mwaka 2020 hadi kufikia dola za Kimarekani 199 mwaka 2021.

error: Content is protected !!