Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza maamuzi ya Kamati ya Maadili kufuatia mashauri dhidi ya maofisa wa klabu za Simba SC na Yanga SC.
Kamati imemtia hatiani Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ally Kamwe, kwa kosa la kuchochea umma kinyume na Kanuni ya 73(4) ya Maadili ya TFF (Toleo la 2021). Kamwe amepigwa faini ya shilingi milioni 5 na kupewa onyo la kutofanya kosa la kimaadili kwa miaka miwili. Adhabu hiyo inaanza rasmi tarehe 16 Aprili 2025.
Kwa upande mwingine, Ahmed Ally, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, ameachiwa huru baada ya Kamati kubaini kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kosa aliloshitakiwa nalo.