Moroni, Comoro – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameeleza dhamira ya Tanzania kuimarisha ushirikiano na Comoro katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, akiitaja changamoto hiyo kuwa ya pamoja kwa mataifa yote ya ukanda wa Bahari ya Hindi.
Akizungumza katika sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Comoro zilizofanyika jijini Moroni, Rais Samia alisema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Comoro katika kulinda mazingira na ikolojia ya bahari kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Comoro ni kisiwa ila Tanzania ni nchi yenye visiwa vidogo, hivyo asi changamoto ya mabadiliko ya tabia nchini inatukabili wote. Mabadiliko haya ya tabia nchi yamepelekea kupanda kwa nyuzi joto, kuongezea kwa maji chumvi ambayo yamekuwa yakila ardhi na kupoteza viumbe wa baharini. Tanzania ipo tayari kushirikiana na Comoro ili kulinda ikolojia yetu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.” amesema Rais Samia.
Mbali na masuala ya mazingira, Rais Samia aligusia pia uimarishaji wa miundombinu ya usafiri kati ya nchi hizo mbili, ikiwemo safari za anga na majini, kama sehemu ya kukuza biashara, utalii na mahusiano ya kijamii.
Aidha, alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa Comoro katika nyanja mbalimbali, akieleza kuwa uhusiano wa mataifa hayo umejengwa juu ya historia, mshikamano na maelewano ya kudumu.
Ziara hiyo ya Rais Samia inadhihirisha kuendelea kwa diplomasia ya Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kushiriki kikamilifu katika juhudi za pamoja za maendeleo endelevu.