Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Tanzania imepanda kwa nafasi tisa katika viwango vya kimataifa vya nchi zinazopendelewa kwa uwekezaji, huku akitoa wito wazi kwa wawekezaji wa kimataifa kuja kuwekeza nchini.
Rais Samia aliyasema hayo Februari 4, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji Afrika (Global Africa Investment Summit – GAIS), unaoendelea mjini Dubai, Falme za Kiarabu.
Alieleza kuwa Serikali yake imejikita kikamilifu katika kuweka misingi imara itakayowawezesha wawekezaji kufanya shughuli zao kwa uaminifu na kwa gharama shindani, akitaja miundombinu ya kisasa kuwa nguzo kuu ya mkakati huo.
Rais Samia alifafanua kuwa miundombinu hiyo haikulengi kuhudumia soko la ndani pekee, bali pia kuiweka Tanzania kama lango muhimu la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, jambo linalozidi kuongeza mvuto wa nchi kwa wawekezaji wa kimataifa.
Aidha, Rais alibainisha kuwa Serikali imetenga maeneo maalum ya kiuchumi mahsusi kwa ajili ya wawekezaji, yanayotoa vivutio mbalimbali vikiwemo upatikanaji wa ardhi ya uwekezaji, nafuu za kodi, pamoja na huduma muhimu zinazotolewa kupitia kituo cha huduma kwa mfumo wa dirisha moja (one-stop service centre).


