Watu saba wafikishwa Mahakamani tuhuma za wizi wa magari ya bandarini

HomeKitaifa

Watu saba wafikishwa Mahakamani tuhuma za wizi wa magari ya bandarini

Watu saba wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kuiba magari mawili yaliyokuwa yakisafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam kuelekea Bandari Kavu (ICD) ya Vingunguti.

Washtakiwa hao ni Isack Natus, Samson Mwamoto, Daniel Noah, Adam Sufian, Michael Wambura Marwa, Fadhil Munisi na Tusho Kalambire. Wote wamekana mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Victoria Mwaikambo.

Upande wa mashtaka umeeleza kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kuiba gari aina ya Nissan Caravan na Toyota RegiusAce, mali ya kampuni ya Sudais Logistic Company Limited, na kuyapeleka eneo la Kigamboni badala ya ICD Vingunguti yalikokuwa yakielekezwa.

Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi, watuhumiwa walikamatwa Agosti 12, 2026 nyumbani kwa mmoja wao, Michael Wambura, huko Kigamboni, pamoja na magari hayo mawili.

Kukamatwa kwao kulifuatia operesheni maalumu iliyolenga kudhibiti wizi wa magari na mizigo inayosafirishwa kutoka bandarini kwenda kwenye Bandari Kavu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 26, 2026 kwa ajili ya kutajwa, huku washtakiwa wote wakiruhusiwa kwa dhamana.

error: Content is protected !!