Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya madini, biashara, uwekezaji, miundombinu pamoja na amani na usalama.
Rais Samia amesema hayo leo Agosti 18, 2026, Ikulu Ndogo Zanzibar, mara baada ya kumpokea Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, akieleza kuwa nchi hizo mbili zina utajiri mkubwa wa rasilimali za madini na hivyo kuna fursa ya kubadilishana ujuzi na uzoefu katika uchimbaji, uongezaji thamani na masoko ya madini.
Amesema katika mazungumzo yao, pia wamegusia masuala ya amani na usalama, ambayo ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya Kanda ya Afrika na dunia kwa ujumla.
Aidha, Rais Samia amesema Tanzania, kama mshirika wa karibu wa DRC, iko tayari kuendelea kushirikiana na nchi hiyo katika kujenga uchumi unaowaunganisha wananchi wa mataifa hayo, kuongeza biashara na uwekezaji, kuboresha miundombinu na kujenga mazingira ya amani na ustawi wa pamoja.


