Wataalamu wa udhibiti na ufuatiliaji wa magonjwa kupitia mbinu ya Epidemiolojia na maabara (TANFLEA) wamesema Tanzania ina uwezo wa kutengeneza chanjo ya UVIKO-19 kutokana na kuwepo kwa miundombinu na uzoefu.
Wataalamu wamezungumza hayo jijini Dar es Salaam ikiwa ni hatua ya kuelekea siku ya Epidimiolojia duniani.
Raisi wa TANFLEA, Dkt. Elibariki Mwakapeje amesema Tanzania ina uwezo wa kutengeneza chanjo ya magonjwa mengine akitolea mfano Chuo Kikuu cha Sokoine kilichopo Morogoro ambacho kiliweza kutengeneza chanjo ya ugonjwa wa Newcastle (Kideri) unaoathiri kuku hapa nchini.
Na chanjo hiyo imeweza kuthibitishwa na vyombo vya kimataifa ikiwemo Shirika la Afya Duniani kwamba chanjo hiyo inafaa na inaweza kutumika. Lakini ukiachana na hilo, Wizara ya Mifugo ina kiwanda cha chanjo kilichopo mkoani Pwani kinachoitwa Tanzania Vaccine Institution kinachotengeneza chanjo ya kimeta, ugonjwa unaosambazwa na mifugo kama ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Sababu nyingine inayoipa Tanzania uwezo wa kutengeneza chanjo ya UVIKO – 19 ni mpango wa chanjo ya taifa ambao umekuwa ukifanya vizuri na tathmini ya miaka 10 iliyopita ya Shirika la Afya Duniani (WHO) limetambua Tanzania kama nchi inayofanya vyema.