Maana ya vitu 7 vya kimila alivyopewa Chifu Hangaya (Rais Samia)

HomeKitaifa

Maana ya vitu 7 vya kimila alivyopewa Chifu Hangaya (Rais Samia)

 

Rais Samia Suluhu Hassan leo ametawazwa na Umoja wa Machifu Tanzania (UMT) kuwa Chifu Mkuu wa machifu wote nchini na kumpa jina la Chifu Hangaya likiwa na maana ya Nyota ya asubuhi inayong’aa. Katika hafla hiyo, Chifu Hangaya amekabidhiwa vifaa vya jadi, ambavyo kila kimoja kina maana yake. Vifaa hivyo ni:

1. Vazi Jeusi
Hii ni ishara ya wingu jeusi la mvua, wingu lenye matumaini ya chakula na kuondoa njaa nchini Tanzania. Kwa vazi hili. Rais Samia kusimikwa kuwa Mkuu wa Chifu, yeye ndio dira ya kuelekea kuhakikisha Tanzania haipati baa la njaa.

2. Vaa Jekundu
Ishara ya damu, kujitoa muhanga, utayari wa hata kufa kulinda watu wake.

3. Ngozi ya Chui
Chui ni mnyama mwenye sifa ya upole, lakini ni mkali zaidi kama utacheza na watoto wake. Ngozi aliyopewa Mama ni ishara ya upole wake, na pia kigezo cha kumwandaa awe mkali kwa yeyote anayecheza na maslahi ya watoto wake (Watanzania).

4. Ushanga uliotokana na mayai ya Mbuni
Mbuni ni ndege mkubwa kuliko ndege wote warukao na watembeao. Mbuni wanasifa ya kuwa wakali sana hasa ukicheza na mayai au vifaranga vyake. Ushanga huo ni ishara ya ulinzi na mapenzi kwa watoto wake (Watanzania)

5. Kiti cha utawala
Kiti cha ukuu. Kiti/kigoda ni ishara ya uongozi na heshima. Maelekezo ni kwamba atatumia kiti hiko kuketi na kufanya maamuzi ya busara ambayo yatakuwa na maslahi mapana kwa watanzania.

6. Ngao na Mkuki.
Yeye kama Amiri Jeshi Mkuu, silaha ni ishara ya ulinzi. Yeye ndio kiongozi kwenye kuhakikisha nchi inabaki salama na mipaka inalindwa kwa gharama yoyote.

7. Usinga
Usinga ni mkia wa ng’ombe. Usinga una nyuzi lukuki, nyuzi hizo ni alama ya idadi ya Watanzania. Usinga unashikwa mkononi na kiongozi wa kimila, hivyo ni ishara ya ulezi na uangalizi. Hivyo mama amepewa jukumu la kulinda na kuwaangalia kwa macho yake yote kama watoto wake.

error: Content is protected !!