Juni 19, 2020, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt John Pombe Magufuli, alimsaidia mwanamke mwenye ulemavu wa miguu kupata bajaji, taarifa tulizozipata ni kwamba bajaji imeibwa.
Nyangoma James amesema kwamba kwa kawaida huwa anailaza bajaji hiyo nyumbani kwa jirani yake ambapo pana ulinzi wa kutosha, lakini kutokana na baba yake (Nyangoma) kuwa mgonjwa, alilazimika kuilaza bajaji nyumbani kwake kwa lengo la kumuwahisha baba yake hospitali, na hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya wezi kuiba bajaji hiyo.
Kwa masikitiko makubwa, Nyangoma ambaye ni mkazi wa Kibaha Kwa Mathias mkoani Pwani, amesema bajaji hiyo ambayo aliinunua baada ya Hayati Magufuli kumpatia shilingi milioni 5 taslimu, ilikuwa msaada mkubwa sana kwake, kwani alikuwa akiitumia kwa ajili ya usafiri lakini pia kama kitega uchumi.
“Mimi nimepata bajaji nikiwa katika mazingira magumu sana. Bajaji imenisaidia katika usafiri wangu mimi binafsi, ninafanya bajaji ndiyo inakuwa kipato changu mimi mwenye cha kuishi na familia yangu. Hapa nilipo nimepanga natakiwa nilipe kodi ilikuwa inatoka kwenye bajaji. Nimeachwa kwenye wakati mgumu, mgumu sana,” amesema.
Nyangoma amewasilisha taarifa za wizi huo kwa mjumbe wa mtaa anaoishi (Kibaha, Kwa Mathias) pamoja na kituo cha Polisi ambapo uchunguzi unaendelea ili kubaini waliohusika.