Mambo yaliyompa Rais Samia nguvu ya kuongoza nchi baada ya kifo cha JPM

HomeElimu

Mambo yaliyompa Rais Samia nguvu ya kuongoza nchi baada ya kifo cha JPM

Leo ni mwaka mmoja tangu Taifa limpoteze aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli kwa ghafla akiwa madarakani hapo Machi 17, 2021, janga lililopelekea kuandikwa kwa historia mpya ya Tanzania.

Pasi na kujiandaa kupokea majukumu ya kuwa Rais wa nchi, makamu wa Rais wa Awamu ya Tano, Samia Suluhu Hassan anatwikwa cheo cha urais na kulazimika kutafuta nguvu za kuhimili uzito wa cheo hicho.

Rais Samia amekuwa Rais mwanamke wakwanza kushika nafasi hiyo huku wengi wakijiuliza kama Je! ataweza kuhimili mikiki ya cheo hicho?

Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuapishwa kwake Machi 19, 2021 Rais Samia amefanikiwa kukisimamia cheo chake sawasawa katika kuikuza nchi na wananchi wake kiuchumi,kisiasa, kidiplomasia, kielimu na kwa ujumla katika sekta mbalimbali nchini..

Lakini Je! ni mambo gani yalimpa ujasiri na umahiri katika uongozi?

Katika mahojiano yake na TBC, Rais Samia ametaja vitu vitatu vilivyompa nguvu ya kuwaongoza Watanzania.

Kwanza, amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa ujasiri kwani yeye ndiye mpanga wa yote na katikati ya msiba mzito akaandaa mazinga ya kupita salama.

Pili, Rais ameitaja katiba ambayo ndio muongozo wa nchi ambayo inamtaka kuchukua nafasi hiyo yeye kama Makamu wa Rais.

Mwisho, Rais Samia ametaja uzoefu wake katika uongozi na majukumu yake chini ya uongozi wa Dkt. Magufuli kuchangia kumjenga kuwa Rais wa Tanzania.

“Nadhani nyie ni mashahidi kwamba mambo mengi hasa yanayohusu nje alikuwa [Dkt. Magufuli] ananitanguliza mimi yeye akishughulika zaidi ndani. Kwahiyo naweza kusema kwamba, kama alinitayarisha vile, alinijenga kwamba chochote kikitokea kuna mtu anaweza akachukua na akaenda nayo.

“Ni uzoefu ambao umenifanya kila kitu nilikuwa najua kinaendeshwa vipi, ukiacha machache, huwezi kujua vyote. Machache sikuwa najua nimejifunza nikiwa katika kiti,” amesema Rais Samia.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi iendelee.

error: Content is protected !!