Dkt. Philemon Sengati aliteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Rais Samia Suluhu Hassan tarehe 15 Mei 2021. Kabla ya hapo amewahi kuwa Mkuu wa mkoa wa Tabora na Mkuu wa wilaya ya Magu mkoani Mwanza. Lakini pia amewahi kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma katika Idara ya Sayansi na Siasa na Utawala wa Umma.
Ikiwa ni miezi takribani Sita tangu Dkt. Sengati ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Sinyanga Ijumaa, tarehe 8 Oktoba uteuzi wake ulitenguliwa rasmi. Dkt Sengati atakumbukwa kwa mengi na wananchi wa Shinyanga lakini kubwa kati ya hayo ni migogoro aliyoingia na wakulima hasa wale wanaolima zao la Dengu.
Ni katika miggoro na wakulima ndipo wakati fulani Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliwahi kutoa dukuduku lake hadharani juu ya Mkuu huyo wa Shinyanga. Dkt. Sengati akiwa Mkuu wa Shinyanga aliwahi kukamata magari zaidi ya 30 yaliyobeba zao la Dengu kwa madai kwa madai ya kukiua masharti ya stakabadhi ghalani, lakini tarehe 10 Agosti, Wizara ya Kilimo kupitia Naibu Waziri wake, Hussein Bashe ilitoa tamko linaloonesha kuwa Dkt Sengati anakinzana na maagizo ya Serikali katika uamuzi aliouchukua.
> Rais Samia ateua na kutengua
“Bashe alisema kuwa alipata malalamiko kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa wafanyabiashara wa mazao wa mikoa ya Mwanza na Mara, wakilalamikia kukamatwa kwa magari yao katika Mkoa wa Shinyanga na kulazimishwa kufuata utaratibu wa kuuza mazao hayo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
Aliongeza kuwa baada ya kupokea malalamiko hayo alimuandikia ujumbe mfupi kwa njia ya simu mkuu wa Mkoa Shinyanga Sengati na kumtaka kuwaachia na kuwaruhusu kuendelea na utaratibu wao lakini alikaidi. Anazidi kueleza kuwa ilipofika Agosti 20, mwaka huu alimwandikia barua akimueleza kuwa katika mkoa wa Shinyanga na baadhi ya mikoa mingine hakuna mfumo wa stakabadhi ghalani hasa kwa zao la Dengu lakini Dkt Sengati aliendelea kukaidi na kupuuza maagizo ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo.
Bashe alisisitiza kuwa jambo hilo haliwezekani, kwani wafanyabiashara wamelipa ushuru stahiki, na wana leseni zote lakini wakifika mkoa wa Shinyanga wanakamatwa huku mamlaka ya namna ya kuuza mazao ikiwa kwa Waziri wa Kilimo pekee na si mkuu wa Mkoa.
Hata Mbunge wa Jimbo la Sumve, Kasalali Mageni aiwahi kunukuliwa katika video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii akieleza kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga (aliyetumbuliwa) amejitangazia uhuru wake na amekuwa Rais kwani anakamata Dengu ya wananchi kinyume cha taratibu. Kasalali alimtaja Mkuu huyo wa mkoa kama jambazi anayepora mazao ya wananchi huku akisema kuwa ni ‘saizi’ yake na atamshughulikia ipasavyo akifika bungeni.
Kwa mtiririko wa matukio haya ni wazi kuwa ukaidi na kutokutii mamlaka zilizo juu yake pamoja na uwepo wa migogoro isiyokwisha kati yake na viongozi wengine ni moja kati ya sababu kuu zilizopelekea Dkt. Sengati kutiliwa mchanga katika kitumbua chake usiku wa tarehe 8 Oktoba 2021 na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Sophia Mjema.