Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na mgeni wake, Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi leo waliongea na waandishi wa habari wakieleza yale waliyozungumza kuhusu ushirkiano wa nchi zao.
Akikaribia kumaliza hotuba yake, Rais wa Burundi Ndayimshiye alisema alieleza kuhusu ulinzi na usalama, ambapo altaja jina la Alexis Sinduhije. Alieleza kuhusu hatari inayotengenezwa na Sinduhije akishirikiana na kundi la ADF. Huyu anayetajwa na Rais mbele ya Rais kama mtu hatari ni nani hasa?
Alexis Sinduhije ni nani?
Mrundi huyo aliyezaliwa Mei 5, 1967, alifahamika zaidi kupitia uandishi wa habari. Kati ya mwaka 1991 na mwaka 1993 alifanya kazi katika redio na televisheni ya Taifa la Burundi kabla ya kwenda kufanya kazi katika magazeti na redio binafsi.
Mwaka 2001, Sinduhije alijizolea heshima na umaarufu baada ya kuanzisha kituo cha redio cha RPA (Radio Publique Africaine) ambacho kilisifika kwa kutangaza amani na umoja katika kipindi cha machafuko nchini humo.
Februari 2003, nyumba ya Sinduhije ilivamiwa na mlinzi wake aliuawa ambapo iliripotiwa kwamba chanzo cha tukio hilo ni habari zilizokuwa zikitolewa kupitia kituo cha RPA. Mwaka huohuo (2003 mwezi Septemba, kituo cha RPA kilifungiwa kwa muda baada ya kufanya mahojiano na msemaji wa kundi la waasi la Agathon Rwasa (National Liberation Forces) lakini kituo cha RPA kilifunguliwa baada ya vyombo vingine vya habari kugoma kupinga kufungiwa kwake.
> Mambo 6 yaliyozungumzwa na Marais wa Tanzania na Burundi
Alexis Sinduhije amewahi kupokea tuzo ya kimataifa ya uhuru wa habari kutoka taasisi ya CPJ (Committee to Protest Journalists) na mwak 2009 jarida la kimataifa la Time lilimtaja kuwa mmoja kati ya watu 100 wenye ushawishi zaidi duniani.
SIASA
Mwaka 2007 alitangaza kwamba atagombea Urais wa Burundi katika uchaguzi wa mwaka 2010. Mwaka 2008 alikamatwa na kushitakiwa kwa kumkashifu Rais wa nchi hiyo (Pierre Nkurunziza), lakini baade alikutwa hana hatia na kuachiwa huru mwezi Machi 2009.
Ndoto ya Sinduhije kuwa Rais haikutimia, mwaka 2010 Nkurunziza alitangazwa kuwa mshindi wa kiti hicho. Kuanzia mwaka huo 2010, Alexis Sinduhije alianza kutajwa katika kundi la wakorofi, kiasi cha kuwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa na Serikali ya Marekani kutokana na vitendo vya uvunjifu wa amani vilivyodaiwa kufanyw ana watu wa chama chake.
Kama ilivyoelezwa leo na Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye mbele ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Burundi inamtambua Alexis Sinduhije kama mtu hatari anayeongoza kundi la MSD (Movement for Solidarity and Development) likidaiwa kuratibu vitendo vya uasi na ugaidi.
Sinduhije anaishi uhamishoni nchini Ubelgiji huku Serikali ya Burundi ikitoa hati ya kumkamata kutokana na tuhuma hizo za ugaidi.