Mfahamu John Okello aliyeshiriki Mapinduzi ya Zanzibar

HomeKitaifa

Mfahamu John Okello aliyeshiriki Mapinduzi ya Zanzibar

John Gideon Okello ni raia wa Uganda aliyeshiriki katika Mapinduzi yaliyoitoa Zanzibar kutoka kwenye minyororo ya utawala wa Waarabu.

Alizaliwa  mwaka 1937 huko Lango, Uganda, akiwa na miaka 11 wazazi wake walifariki akabaki akilelewa na ndugu zake. Alipofikisha miaka 15 aliondoka nyumbani na kuanza kujitegemea, Okello alikuwa mzurulaji kipindi hicho cha ukoloni wa Waingereza Afrika Mashariki akifanya kazi mbalimbali kama ukarani, kufagia na kulima bustani za maua katika nchi za Kenya na Tanganyika.

Mwaka 1959 baada ya kumaliza kutumikia kifungo cha miaka miwili kwa makosa ya ubakaji nchini Kenya, Okello alitimkia kisiwani Pemba na kuwa mkulima na kujiunga na ASP iliyokuwa ikiongozwa na Hayati Sheikh Abeid Karume, kutokana na  msimamo wake na hotuba zake zilizokuwa zikilaani ukoloni wa muingereza Afrika Mashariki na utawala wa Waarabu wachache Zanzibar alipata umaarufu ndani ya chama hicho.

Mwaka 1961, Okello aliwasiliana na viongozi wa ngome ya vijana wa ASP kupanga namna yakung’oa utawala wa Sultani. Mbali na kuwa mkulima Okello pia alikuwa mpaka rangi maarufu aliyesajiriwa na Umoja wa wapaka rangi wa Zanzibar hivyo alitumia mshahara wake aliokuwa akilipwa na umoja huo kuzunguka Visiwani kwenye matawi ya chama ili kushirikiana na viongozi ww ASP kwenye mipango ya Mapinduzi.

Alishiriki katika kujenga jeshi dogo la vijana shupavu ambao inasemekana kwamba walifuata masharti makali ya kujiimarisha ikiwemo kutokufanya mapenzi, kutokula nyama na kutokunywa pombe.

Tarehe 12 Januari mwaka 1964, Okello alikuwa miongozi mwa wanamapinduzi waliovamia Stone Town, mji mkuu wa Zanzibar. Licha ya kuwa na silaha chache walifanikiwa kuwapiga askari wa serikali na kumpindua Sultani.

error: Content is protected !!