Kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) mwaka 2019/2020 wanafunzi 6,654 wa vyuo vikuu waliacha masomo ambapo wanafunzi 4,178 waliacha masomo kwa kushindwa kukidhi vigezo vya kitaaluma, 1,261 kwa kufutiwa usaili, 938 kwa sababu ya utoro, 205 kuahirisha masomo na vifo 72.
Idadi hiyo ni kubwa na inaonesha ongezeko kutoka mwaka 2018/2019 ambapo idadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu walioacha masomo ilikuwa 6,654.
Zipo sababu nyingi zinazopelekea wanafunzi wa vyuo vikuu kuacha masomo. Baadhi ya sababu hizo ni;
5. Uhuru uliopitiliza
Inaamika kwamba mtu anapofika Chuo Kikuu anakuwa ni mtu mzima kiasi cha kutosha kujisimamia mwenyewe. Hivyo, hakuna utaratibu mzuri wa kufuatilia tbaia na mwenendo wa wanafunzi wawapo vyuoni tofauti na ilivyo katika shule za sekondari.
Kutokana na hili, wanafunzi wengi wa vyuo vikuu huingia katika tabia hatarishi na mambo mengine yanayowafanya washindwe kujikita katika masomo.
4. Msingi mbovu katika ngazi ya sekondari
Mfumo wa masomo katika vyuo vingi nchini, huhitaji wanafunzi kujituma sana wao wenyewe badala ya kutegemea kulishwa vitu vingi na walimu wao.
Wahadhiri wengi katika vyuo vikuu nchini wanaeleza kwamba, wanafunzi wengi wanakosa msingi bora wa kuendana na kasi ya masomo katika vyuo vikuu kwa sababu elimu ya sekondari haikuwaandaa vyema.
3. Uchaguzi mbaya wa kozi.
Baadhi ya wanafunzi huingia vyuo vikuu na kuanza kusoma masomo ambayo hawayamudu.
Hili husababishwa na wao kushindwa kuchagua vyema au wakati mwingine kupangiwa (na Tume ya Vyuo Vikuu) katika kozi ambazo hawazimudu. Matokeo yake, baadhi wameshindwa kuendelea na masomo hayo.
2. Matatizo ya kiuchumi
Baadhi ya wanafunzi wanaotoka katika familia zenye kipato duni, wameshindwa kuendelea na masomo hususan baada ya kukosa mikopo au kwa kupata kiwango kidogo kisichoweza kukidhi mahitaji yao ya msingi.
1. Rushwa ya ngono
Utafiti wa rushwa ya ngono katika taasisi za elimu ya juu uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) umebaini upungufu kwenye mifumo ya utahini inayotoa mwanya kwa wahadhiri kutumia vibaya mamlaka yao.
Rushwa ya ngono inatajwa kama moja ya sababu zinazopelekea wanafunzi wengi hususan wa kike kuacha masomo. Pale wanapowakataa wahadhiri wao hufelishwa mitihani na hivyo kushindwa kuendelea na masomo.
Chanzo – Gazeti la Mwananchi (Novemba 1, 2021)