Zifahamu dalili 6 za matapeli mtandaoni

HomeElimu

Zifahamu dalili 6 za matapeli mtandaoni

Maendeleo ya Sayansi ya Habari na Mawasiliano kwa kiasi kikubwa yamefanya mapinduzi katika sekta mbalimbali kama biashara, usafirishaji na kadhalika. Tumeshuhudia na bado tunaendelea kuwa mashuhuda wa maendeleo makubwa katika sekta ya biashara kuanzia mwisho mwa karne ya 20 hadi katika karne hii tuliyonayo, karne ya 21.

Ukosefu wa elimu au uelewa wa kutosha kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia, umegharimu sana maisha ya watu ikiwemo kupata hasara kwenye biashara ikiwemo upotevu mkubwa wa fedha. Hivi karibuni kumezuka wimbi kubwa la watu wanaolalamika kuhusu kutapeliwa kwa njia ya mtandao, ambapo huko hukutana na watu wanaojitambulisha kama wafanyabiashara, huku ikiwa malengo yao ni ghilba na kuiba fedha za watu kwa njia za kitapeli. Sasa mpenzi msomaji wetu, utawajuaje matapeli kupitia mtandaoni?

Ukiona dalili zifuatazo unapaswa kuwa makini zaidi.

1. Hutumia picha zilizopakuliwa (downloaded)
Mara nyingi wezi wa mtandaoni hupenda kutumia picha zilizohaririwa vizuri ambazo huvutia macho ya mtazamaji kwa haraka zaidi. Picha hizi watu hao huzipakua kutoka mtandaoni na zinakuwa hazipo kwenye miliki yao, yaani sio wao waliozipiga. Picha hizi hutumiwa kuvutia wateja, na ukichunguza vizuri, utakuta picha moja imetumika na zaidi ya wafanyabiashara 10 katika mitandao tofauti au mtandao mmoja.

2. Akaunti kuwa ‘private’
Matapeli hawa mara nyingi huweka akaunti zao faragha, Hutawahi kuifikia ili kuona marafiki au picha za familia. Wanajaribu kuwa wasiri kuepuka kugundulika au hata watu wao karibu, familia zao na maeneo wanayoishi. Uonapo akaunti ya mtu anayejinadi kuwa mfanyabiashara mtandaoni huku ukurasa wake ukiwa faragha, ni vyema ukawa makini zaidi.

3. Hufanya biashara ‘private’
Ukiacha kufanya majadiliano na mfanyabiashara usiyemfahamu mtandaoni ni vyema ukaanza kuwa makini mapema kabisa. Ukiona anaanza kukuambia njoo faragha kama vile WhatsApp, Telegram ni vyema ukaongeza umakini zaidi. Sio wote wenye kufanya hivyo ni wezi, lakini kama ni biashara kati ya mteja na muuzaji ikifanyika kwa uwazi katika uwanja wa comments inaongeza imani ya wateja wengine.

4. Huwa na bidhaa chache
Mara nyingi matapeli wa mtandao huwa na mzigo hafifu na hata katika kurasa zao hupenda kuweka maelezo kwamba “mzigo umebaki mchache”. Lengo la kufanya hivi kumtia mteja tamaa na wasiwasi kwa muda mmoja. Kwanza kwakuwa mzigo ni mchache hivyo usingependa kukosa, hivyo mteja analazimika kutuma pesa mapema apate kuhifadhiwa mzigo wake. Kitendo cha kutuma fedha hiyo kabla hujapata mzigo wako, kuna asilimia zaidi ya 95% ya kutapeliwa.

5. Bidhaa zao huwa za bei ya chini
Tapeli anajua watu wako tayari kuhatarisha pesa kidogo, kwa hivyo bei zao huwa chini kila wakati. Hiki ni chambo tu cha kukuvutia kabla ya kumeza ndoano. Hili ni jambo la kawaida kwani hufanya hivi hili usiende sehemu nyingine na kuishia kwao.

6. Hawana anwani ya sehemu yao ya biashara
Moja ya dalili za matapeli wa mtandaoni ni kutokuwa na anuani ya eneo husika ambapo biashara zao hupatikana. Sababu kubwa ukiuliza kutaka kujua watakwambia wanafanya kazi nyumbani. Ikumbukwe kwamba unapaswa kuongeza umakini kwa mfanyabiashara kwenye majibu ya namna hii. Htata hivyo, si wote wafanyaobiashara nyumbani ni matapeli, ingawa kuongeza kuongeza umakini ni jambo sahihi zaidi.

error: Content is protected !!