Filamu hii inawahusu mabinti watano ambao kwa mara ya kwanza wanakutana katika moja ya hoteli iliyopo Cancun mjini Mexico.
Kila mmoja akiwa na dhumuni binafsi la kwenda sehemu hiyo. Moja wapo ikiwa ni kutoa stress za maisha kwa burudani ya muziki inayotolewa na bendi mashuhuri hotelini hapo.
Wakati kila mtu akiendelea na shuguli zake, ghafla linapita tetemeko la ardhi linalofanya watu wote waliopo katika eneo hilo wakusanyike kwenye fukwe za bahari zilizopo pembezoni mwa hoteli hiyo .
Wakiwa huko binti mmoja anagundua kuwa jirani yake ana kitu ambacho hata yeye anacho.
Ni alama ya kuzaliwa yenye umbo la samaki. Wakati wawili hawa wakiulizana imekuaje wakawa wana alama hiyo iliyofanana, binti aliekuepo kando yao anawasikia wanachozungumza na kuwaeleza kuwa hata yeye ana alama hiyo hiyo.
Wakiwa katika sintofahamu, anakuja binti mwingine na kuwaeleza kuwa boyfriend wake amewasikia wanazungumzia alama ambayo hata yeye anayo.
Mabinti hawa wanageukiana na kutazamana wakionekana kustaajabu kwa wanachokiona,.
Wakiwa hawaelewi cha kufanya, mmoja wao anaamua kuuliza kwa sauti katika umati uliokuepo.
‘Kuna mtu ana alama ya kuzaliwa yenye umbo la samaki?’
Umati unastaajabu ni nini binti huyo anazungumza, lakini inasikika sauti katikati ya umati huo.
‘Mimi hapa ninayo’ huku binti mmoja akijitokeza na kuwaonesha alama hiyo, wanajikuta wote wamekaa chini kwa kuishiwa nguvu za miguu.
Inawezekanaje hii? Mabinti wote hao wawe na alama moja tena katika eneo moja. Jibu hawana, cha msingi wanaamua wajuane hata majina lakini ajabu ni kuwa hata kujuana kwao majina kunazidi kuwamaliza nguvu.
Wote majina yao ni Juana. kuna Juana Valentina, Juana Maltilde, Juana Bautista, Juana Manuela na Juana Caridad.
Wanazidi ‘kupagawa’ kabisa na wanapoulizana kuhusu wazazi, wote wanajikuta kuwa hawajawahi kutana na baba zao.
Unaweza kusema “destiny” imewakutanisha mabinti hawa, lakini kumbe kuna siri iliyojificha kama nyoka aliyepo kwenye majani.
Mabinti hawa au tunaweza waita Juanas, wanaamua kujua kinaga ubaga juu ya alama walionayo, huku jambo linalowatilia shaka ni kwanini mama zao waliwaficha kuhusu baba zao.
Wakiwa katika harakati zao za kuutafuta ukweli Valentina anashauri wakapime DNA, na majibu yanapotoka yanaonesha kuwa mabinti hao ni wa baba mmoja.
‘Kimbembe’ kinabaki ni nani huyo? Na kabla hawajapata jibu, Bautista ambaye ana kipawa cha kusoma nyota anawaambia kuwa baba yao ndiye muhusika wa vifo na taabu zote za mama zao.
Jambo hilo linawazidishia hasira na kuongeza kasi ya upelelezi wao. Siku si nyingi baada ya mihangaiko wanakuja kumjua baba yao.
Ni Simon Marroquin. Kigogo wa serikalini ambaye anawania nafasi ya ‘mwanasheria mkuu’, na kwa upande wake hajui kama ana mabinti watano kutokana na tabia yake ya kubadilisha wanawake.
Inakuwa kama sukari imeangukia kwenye chai kwani wakiifichua siri hiyo hadharani basi utakuwa ni mwisho wa kigogo huyo.
Lakini ukweli huo unakuwa mchungu kwa Valentina ambaye ameshazama kwenye penzi zito na Federico, mtoto pekee wa kiume wa Simon, kwa maana hiyo Valentina yupo kwenye mahusiano na kaka yake bila kujua.
Binafsi siwezi hata vuta picha vile ningekuwa nimechanganyikiwa.
Kwa upande wake Manuela anakuja kujua kuwa mke wa Simon, Catalina ni dada wa mama yake, ikimaanisha kuwa mama yake alikuwa kwenye mahusiano na mume wa dada yake.
Kiufupi siri moja inazidi kuleta siri nyingine, ambazo zinawaumiza mabinti hao na kufanya wachanganyikiwe.
Jambo linalowaumiza akili mabinti hawa wenye kiu ya kisasi ni kukosa ushahidi utakao wasaidia kumuangusha baba yao.
Fuatilia filamu hii ya muendelezo iliyobeba kisa cha kusisimua kupitia jukwaa la filamu la mtandaoni la Netflix.